Mada hii iliwakilihwa na Carol Thompson jumatano tarehe 09/07/2008 na iliweza kuibua mjadala mkali kutoka kwa wana-GDSS. Mwezeshaji aliweza kutoa historia ya Vurugu zinazoendelea sasa na alizihusisha na vyanzo vikuu vitatu, ambavyo ni Mgogoro wa Kiuchumi, Kikatiba na Kiuongozi. Mgogoro kiuchumi ulianza kabla ya vurugu zinazoendelea sasa baada ya rais Robert Mugabe kufanya marekebisho ya sera ya ardhi mwaka 2000, ambayo yaliwapa Wazimbabwe weusi haki ya kumiliki ardhi iliyochukuliwa zamani kwa mabavu na wazungu. Mabadiliko hayo yalisababisha mataifa tajiri yakiongozwa na Marekani na Uingereza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi serikali ya Zimbabwe, na hapo mgogoro wa kiuchumi ukaanza. Huduma muhimu zikakosekana kabisa, afya, elimu, chakula, na mfumuko wa bei uliovunja rekodi ya dunia na kufikia 1000% kwa siku. Wazimbabwe zaidi ya milioni 3 wameshakimbia nchi yao kutokana na njaa na uoga walionao juu ya mstakabali wa maisha yao mpaka sasa, wanawake na watoto wakiwa ni kundi liloathirika zaidi katika dhahama hii.
Mgogoro wa kikatiba ambao nao umechangia vurugu zinazoendela ulianza baada ya Marekebisho ya kitiba ya Zim yaliyofanywa na serikali ya Mugabe mwaka 2002. Marekebisho hayo yalimpa rais mamlaka makubwa na kumfanya awe juu ya sheria na mwenye madaraka yote ya nchi, hata bunge la nchi halina uwezo wowote juu ya rais. Marekebisho haya ya katiba yamesababisha kusiwepo na mfumo mzuri wa uchaguzi huru na wa haki kitu ambacho kimechangia kuwepo kwa machafuko ya kisiasa.
Mgogoro wa kiungozi umechangia pia kuwepo kwa machafuko yanayoendelea hivi sasa. Kutoelewana kati ya viongozi wa chama cha upinzani cha MDC, Bw. Morgan Tshangirai na Bw Mutambara kumechangia kukua kwa mgogoro huu. Tshangirai anamtuhumu Mtambara kwa kufanya majadiliano na Mugabe juu ya kuunda kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kitu ambacho kwa mujibu wa Tshingirai ni usaliti kwa Wazimbabwe. Pia kuna swala la mkanganyiko kuhusu uwakilishi wa chama cha MDC, kwa upande mmoja kinaonekana kama kinawakilisha wafanyakazi na kwa upande mwengine kinawakilisha mabepari, kitu ambacho kinazua hofu miongoni mwa wafuasi na wasio wafuasi wa chama hiko.
Uchaguzi wa tarehe 27 June, 08 uliendeleza tuu vurugu ambazo zilishaanza kuota mizizi tangu awali. Viongozi wa Umoja wa Africa na SADC walikubaliana kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki, na ulikuwa na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu. Lakini mpaka sasa viongozi wa Afrika wamegawanyika katika makundi mawili juu ya mgogoro huo, la kwanza ni lile linakubaliana na uumuzi wa serikali ya Mugabe na la pili ni lile linalomuona Mugabe ni chanzo cha matatizo yote yanayotokea Zimbabwe. Vurugu zinazoendelea zitaweza kukwamisha mazungumzo yanayoendelea katika kujaribu kuleta serikali ya umoja wa Kitaifa, na pia uchumi wa nchi kuanguka kabisa kitu ambacho kitaongeza machungu kwa wananchi maskini hasa wale wa vijijini.
Michango ya wana-GDSS iligawanyika katika makundi mawili, wapo waliomtetea Mugabe na sera zake na wapo waliomuona kama ni chanzo cha matatizo yote haya na ilipaswa awajibishwe kwa maslahi ya wananchi wa Zimbabwe. Makundi yote yanaweza kuwa hoja za kushawishi, lakini kinachotokea Zimbabwe sasa yapaswa kiunganishwe na chanzo chake halisia; kipindi cha awali wakati wa uvamizi wa mabepari wa kiingereza walipochukua kwa mabavu ardhi ya waafrika na kujimilikisha. Uhuru wa Mwaka 1980 uligusia kurudisha ardhi hiyo kwa Waafrika pindi hali ya kisiasa itakapotengemaa, kitu ambacho hakikutekelezwa mpaka Mugabe akaamua kuwafukuza wazungu kwa nguvu. Mapambano yanayoendelea sasa Zimbabwe ni muendelezo wa Waafrika katika kupinga uvamizi wa mataifa ya kibepari-ubeberu katika rasilimali za Afrika. Wana-GDSS wakajiuliza migogoro mingapi ambayo itatokea katika nchi za Afrika endapo Waafrika wataamua kuungana na kudai rasilimali zao zilizo na zinaporwa na mataifa ya Kibepari-ubeberu katika siku zijazo?
4 comments:
Kilichojadiliwa wiki iliopita kilikuwa ni muhimu sana kwetu (waafrika) na hasa sisi watanzania.
regardless ya nini alichoongea mtoa mada wetu kuhusu zimbabwe, lakini pia ilijionyesha wazi katika mjadala ni jinsi gani watanzania wana taarifa na ufisadi na unaofanywa na mabeberu kwa rasilimali zetu za afrika.
mugabe kama rais alifanya kile alichokiona sahihi kwake katika mwelekeo huo huo wa 'kurudisha rasilimali kwa wananchi'.
kinachoendelea sasa na hali halisi ya zimbabwe leo hii, ni matokeo ya huo huo ubeberu ambao mekuwa ukipambana na mugabe kwa namna tofauti tofauti, ikiwemo kuiwekea zimbabwe vikwazo vya kiuchumi!!
sio siri, nchi nyingi za kiafrika (kama sio zote) uchumi wetu ni tegemezi, na mbaya zaidi tunawategemea hao hao mabeberu 'watutegemeze' - HAPO NDIO NGOMA INAPOKUWA NZITO!!
salma
Mugabe yuko sahihi wazungu wasimuingilie siasa za Zimbabwe.
Mwasiti
Upendo Group
mugabe sio beberu kama watu wanavyodhani bali ni upotoshwaji wa wazungu ambao siku zote hawaitakii mema afrika
pamoja na mambo yote kuhusu zim, kwangu mimi naona zim ndio mstari wa mbele katika mapambano ya unyonyaji mambo leo unaoendelea afrika na dunia kote, ambao unaendeshwa na mabeberu wakuu wa dunia hii wakiongozwa na marekani na uingereza. Ingekuwa zim ina nguvu kidogo basi mugabe angeondolewa na kwa bunduki lakini ni masikini ndio wanatumia vi-mbinu-mbinu vya hapa na pale.
Wafrika wanapaswa waungane ili wafanye ukombozi wa kweli wa mali na watu wake.
denyo
Mwanaharakati
Post a Comment