15/07/2008
Tumepokea na kufuatilia mkanganyiko wa sababu za kifo cha mama mjamzito (Teddy Dimoso) na kichanga wake wakati wa kujifungua kwa masikitiko makubwa sana. Kwa mujibu wa barua kutoka kwa msimamizi wa mirathi kifo hiki kilitokea tarehe 01/06/2008 katika hospitali ya Mwananyamala. Barua hiyo ya tarehe 06/06/2008 kwenda kwa Waziri wa Afya inatoa maelezo kwa kina jinsi kifo hicho kinavyoweza kuwa kimetokea kwa uzembe.
Vyombo vya habari viliripoti kuhusu utawala wa Hospitali ya Mwananyamala na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam walivyokuwa wakitoa majibu yasiyoridhisha na yanayojikanganya juu ya kifo hicho. Mbali na Wanaharakati kudai iundwe tume huru kuchunguza mazingira ya kifo hicho na kutoa usahihi wa yaliyojiri, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam aliamua kuunda tume bubu tarehe 18/06/2008.
Kwa mtazamo wetu tume hii ilikuwa na mapungufu yafuatayo; Wajumbe wake hawakujulikana hadi tarehe 11/07/2008 Kandoro alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu ripoti yao. Wananchi hawakutangaziwa hadidu rejea za tume hii. Wananchi hawakutangaziwa tume itafanya kazi kwa muda gain na katika ofisi gani ili walio na maoni au ushahidi wapate kupeleka. Wajumbe wa tume hii wote ni watendaji wa serikali, hivyo kulikuwepo mgongano wa maslahi. Tume imetoa maelezo yale yale ambayo Mkuu wa Mkoa alikuwa akitoa kila siku, hivyo kutia shaka kama watu wote waliohusika na kushuhudia tatizo hilo wanafikiri kama Kandoro. Huu ni ushahidi wa usanii wa Kisiasa uliotukuzwa.
Kwa mujibu wa nakala ya taarifa kwa vyombo vya habari tarehe 11/07/2008 toka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam bado usahihi wa sababu za kifo cha marehemu Tedy Dimoso haujapatikana. Kwenye taarifa hiyo hakuna kabisa maelezo kutoka kwa ndugu wa marehemu na wala Mkuu wa Mkoa haonekani kuguswa na kifo hicho. Mkuu wa Mkoa pia hajawahi kuwasiliana na ndugu wa marehemu tangu kifo hicho kitokee.
Mkanganyiko wa maelezo uliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na hospitali ya Mwananyamala na namna jambo lenyewe lilivyoshuhulikiwa inatia mashaka makubwa. Femact bado tuanadai usahihi wa kilichotokea na kutaka haki itendeke pande zote mbili; upande wa marehemu na upande wa hospitali. Sisi tunadai masuala mahsusi kabisa siyo kinyume na majibu haya ya kisiasa.
Tunahitaji Mkuu wa Mkoa atoe ufafanuzi wa haya yafuatayo;
• Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hospitali ya Mwananyamala ilipangiwa pesa za dawa peke yake shilingi 174,502,463 katika mwaka wa fedha 2007/08. Ni kiasi gain cha pesa hizi zilitumika? Kwa nini Tedy Dimoso alifariki kwa kukosa dawa?
• Kwa mujibu wa Mpango wa Utoaji huduma za Afya (CCHP) wa Manispaa ya Kinondoni mwaka wa fedha 2007/08, Hospitali ya Mwananyamala ilipanga kutumia shilingi 22,000,000 kugharamia dawa na vifaa vingine kwa kitengo cha Uzazi hospitalini Mwananyamala. Ni kiasi gani cha pesa hizi zilitumika mwaka wa fedha 2007/08?
• Pia Hospitali ya Mwananyamala ilitengewa shilingi 210,000,000 kujenga jengo la ghorofa moja kwa ajili huduma za mama na mototo katika hospitali ya Mwananyamala. Ujenzi wa jengo hili umefikia wapi? Kwa nini Tedy Dimoso alifanyiwa upasuaji wodini?
• Kwa mujibu wa Mwongozo wa Utekelezaji wa Sera ya Wananchi Kuchangia Gharama za Huduma za Afya katika Hospitali ya mwaka 1994, mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanastahili kupata huduma za afya bure bila malipo. Kwa nini ndugu wa marehemu Tedy dimoso waliambiwa wakanunue dawa?
• Kwa mujibu wa kifungu namba 14 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 toleo la 2005, kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake. Kwa nini serikali haikutimiza wajibu wake wa kutunza na kuhakikisha uhai wa Tedy Dimoso?
Tunahitaji kuona Mkuu wa Mkoa anafanya yafuatayo;
• Anatupilia mbali ripoti ya tume yake bubu na kuunda tume huru kuchunguza matatizo na vifo vya mama wajawazito na watoto chini ya miaka 5 katika Jiji la Dar es Salaam. Mama wote waliojifungua tangu January 2007 (au ndugu wa marehemu) ni vizuri wakahusika kuhojiwa.
• Mkuu wa Mkoa anaomba radhi kwa wananchi wa Manispaa ya Kinondoni kwa dharau aliyoonesha wananchi wanaolijua tatizo hili kwa kina pamoja na ndugu wa marehemu
• Mbunge wa Kinondoni anaomba radhi wapiga kura wake kwa kutoa kauli potofu Bungeni kuhusu tatizo hili.
• Mkuu wa Mkoa anawajibisha wote watakaobainika kuhusika na uzembe huo
• Mkuu wa Mkoa na Manispaa ya Kinondoni hawatumii vitisho na propaganda kutisha wananchi wanaojaribu kutetea haki na uhai wa wananchi
• Nakala za mpango kazi na bajeti ya utoaji huduma kwa kila Hospitali, Kituo cha Afya, na Zahanati zibandikwe sehemu ya wazi wananchi na wahudumu wa afya wafuatilie.
Imetolewa na Wanaharakati wa mtandao wa haki za binadamu na jinsia (FEMACT) na Kusainiwa na
Ms. Usu Mallya
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP
Kwa niaba ya FEMACT
6 comments:
ukweli mwananyamala ni wazembe sana manesi kuzarau wagonjwa hata unpoitaji msaada hawakusikilizi ka
bisa
Nuru Luksasi
upendo group
tatizo kubwa ni ueliwa kwa wakinamama kujua akizao naiomba silekali kutoa elim yakutosha kwa wakinamama kujua akizao zamsingi katika matibabu ya wakinamama wakati wakugifugua katika zanati zoti mgin na vigigini yasitoke tena kamaayo ya kinodoni ya binti alikufa sababu ya elufu sita ya matibabu asati
jumanne mzungu
kifupi si mwananyamala pekee bali ni hospital za serikali wahudumu wake hawafuati maadili ya kazi
Nuru Luksasi
upendo group
Maoni yangu kuhusu kifo cha mama mjamzito katika hospitali ya mwananyamala hivi karibuni, sio tu uzembe bali ni matatizo ya mahospitali mengi ya serikali na hata yale ya binafsi. Hospitali nyingi zinatoza gharama kubwa mno na pia watendaji wao yani madaktari na manesi hawajui kazi zao na wajibu wao vyema na hii inachangia tatizo kama hilina watu kufariki bila sababu.
Tatizo hili limeanzia mbali kwa maana kuwa serikali yenyewe haiko makini kufatilia na kusimamia mahospitali na watendaji wake, pia hawako makini kusimamia maswala ya madawa, kuna kisa kimoja mtu aliandikiwa dawa na daktari akaenda phamacy kununua dawa aina ya tetracyclin akachukua dawa akatumia lakini akazidi kuumwa, matokeo yake alirudi kwa daktari na kumweleza yaliyojiri,akambadilishia dawa,bahati nzuri akapata nafuu.
zile dawa za zamani kumbe hazikua dawa bali ndani yake kulikua na unga wa mhogo.
Ina maana kuna viwanda vingi vya uchochoroni vinavyotengeneza dawa za watu, hili ni jambo kubwa sana na la hatari serikali inapaswa kuwa makini nalo.
Kwa sasa dawa nyingi kutoka India ni feki kuna mama mmoja namjua amepata infection ya kawaida tu UTI ametibiwa kwa muda wa miezi minne hajapona UTI. Tujiulize ni kwanini? ina maana dawa alizokuwa akipewa si dawa bali ni dawa feki. mama huyu alipona kwa kutumia dawa za mitishamba katika kitengo cha dawa asilia cha Muhimbili.
Tatizo hili linatufundisha nini, ni kwamba kuanzia katika Wizara ya afya kote kunakohusiana na jambo hili ni kwa kurekebisha na kwa makini.
Biashara huria imeleta madhara makubwa kwani kila mtu analeta biashara anayoitaka na wale wanaosimamia taratibu zote wanapewa 10%(ten percent) wanakaa kimya dawa feki zinaingia mitaani na wananchi wanateseka. Corruption nayo iko mbele katika tatizo hili.
Hospitali ya Mwananyamala wangeondolewa wafanyakazi wote wapelekwe sehemu tofauti na wapewe onyo kali kwa kuwa lazima wanashirikiana katika kazi zao za kizembe, na wale waliohusika na kifu cha yule mama washtakiwe na wasiruhusiwe kufanya kazi popote TZ
Mimi binafsi nilishashuhudia mgonjwa amekuja dirishani kuchukua dawa alioandikiwa na dokta, yule mfamasia wa pale hospitali alikua anaongea na simu, akamwashiria alipo dirishani kwamba wewe nenda hakuna dawa, wakati zipo! mgonjwa akaondoka zake, sasa hii ndo nini uzembe na kukosa ubinadamu.
Pale hospitali pia hawajui kutoa kipaumbele kwa wagonjwa waliozidiwa wote wanawatreat the same, ni makosa sana, wazee hawapewi kipaumbele nk. hili ni tatizo pana na linahitaji busara nyingi kudili,pamoja Nchi yetu ni masikini japo tupo 3rd world bado tuna safari ndefu sana kulitekeleza tatizo hili kubwa.mwisho
Milly mchaki
Mshangao theatre
Ukweli viongozi wetu niwazembe sana kamaserikali ingekuwa inatilia mkazo wazazi wa sidaiwe rushwa ya aina yeyoteile huyomzazi aliye kufa hapo sababu ni nini?kama siyorushwa mishahara duni inazalisha rushwa, rushwa inazalisha vifo kwa wazazi naiomba wizala ya afya wasibaki ofisini iombe bajeti kubwa ili wazazi wapone. Mimi Mwanafunzi Shaghufta Msangi Magomeni S/School
Ukweli viongozi wetu niwazembe sana kamaserikali ingekuwa inatilia mkazo wazazi wa sidaiwe rushwa ya aina yeyoteile huyomzazi aliye kufa hapo sababu ni nini?kama siyorushwa mishahara duni inazalisha rushwa, rushwa inazalisha vifo kwa wazazi naiomba wizala ya afya wasibaki ofisini iombe bajeti kubwa ili wazazi wapone. Mimi Mwanafunzi Shaghufta Msangi Magomeni S/School
Post a Comment