Utangulizi.
Blogi hii itakuwa na sehemu ya mohojiano ya ana kwa ana na wanaharakati mbalimbali ambao ni wanachama wa GDSS wakitueleza historia yao kwa ufupi, kazi wanazojishughulisha nazo, changamoto wanazikutana nazo, ushiriki wao wa GDSS, na faida walizozipata kutokana na ushiriki huo. Lengo la mahojiano haya ni kupata uzoefu kutoka kwa wanaharakati wengine na kujifunza kutokana na uzoefu huo.
Wiki hii tulipata bahati ya kufanya mahojiano mafupi na Bw. Albert Killango –Afisa Mipango wa asasi ya Precious Jewels Organization (PJO Tanzania) yenye makazi yake Mabibo Dar es Salaam. Ambaye alieleza historia yake ya harakati iliyoanzia alipokuwa shuleni mwaka 1996/7, walipoanzisha kikundi cha vijana cha Barcelona Family kilichojihusisha na maswala ya Michezo na Burudani. Mwaka 1998 akakutana na mama Ichikaeli Maro ambaye alimtambulisha TGNP na hapo alianza rasmi safari yake ya harakati. Semina za kwanza kwanza anazozikumbuka ziliwezeshwa na Richard Mabala, dada Ussu Mallya, na zilikuwa zinahusu VVU na Vijana na Mafunzo ya Uongozi katika asasi na Vikundi unaozingatia usawa wa kijinsia. Mafunzo hayo yalimuwezesha yeye na
wanaharakati wengine kuunda kikundi cha kupambana na UKIMWI kilichoitwa Tumaini Youth Movement mwaka 1999. Tumaini iliweza kuandaa na kufanikisha programu kadhaa za UKIMWI ndani ya wilaya ya Kinondoni, mojawapo ni Cheza Salama na HIV iliyofadhiliwa na UNICEF, ambayo ilihusu kutoa elimu ya UKIMWI kwa njia ya Matamasha ya wazi ya Burudani.
Mwaka 2005 waliona kuna haja ya kupanua wigo wa utetezi wa haki za kijamii na kuboresha maisha ya walio pembezoni, hivyo wakaanzisha rasmi asasi ya Precious Jewels Organization (PJO Tz) kwa lengo la utetezi wa haki za wanajamii hasa walio pembezoni.
Kaka Killango anasema kwamba “kuna faida nyingi nilizozipata kutokana na ushiriki wangu wa GDSS”, alizitaja baadhi ni; kuweza kupata elimu na ujuzi mbalimbali kupitia mada, mijadala, na shughuli za GDSS. Mfano wa ujuzi ni uwezeshaji (facilitations skills), ushawishi na utetezi, uongozi wa asasi na vikundi, na elimu ya usawa wa kijinsia. Ujuzi huu umemwezesha kusaidia jamii iliyomzunguka katika kutafuta suluhisho la matatizo mbalimbali, kwa mfano mwaka 2004 walitetea kufunguliwa kwa maji katika mitaa ya Jitegemee, Kanuni na Azimio, baada ya viongozi wachache wa serikali za mitaa na wafanyabishara kuyafunga ili waweze kuuza maji yao ya kibiashara.
Pia ushiriki wake katika semina hizi umemsaidia kuweza kujiamini, kujenga hoja na kuitetea mbele za watu mbalimbali. Kusimama katika majukwaa tofauti na kuongea kumjengea imani ya kuamini kama naye pia anaweza, kitu ambacho kwa maneno yake mwenyewe anasema “mwanzoni hakikuwepo ndani yangu”
Tatu, kupata Mbinu tofauti za kupambana na Matatizo na Changamoto zinazotokea katika maeneo yake kwa kusikia ama kujifunza kutoka kwa wengine jinsi wanavyotatua matatizo yanayofanana na hayo yanayowakabili. Visa mkasa vinavyotokea katika maeneo mengine na kuwakilishwa na wanaharakati vinasaidia kupata mbinu za kutatua matatizo yanayotokea katika eneo lake.
Semina pia zimempa fursa ya kutandaa (Networking), kitu ambacho anasema kimempa faida kuu mbali. Kwanza kupata taarifa mbalimbali muhimu, na pili kuweza kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja na wadau na asasi zingine. Mfano kwa sasa yupo katika Mtandao wa kufuatilia utekelezwaji wa bajeti ya afya na Ukatili wa Kijinsia wilayani Kinondoni ambao unajumuisha asasi kumi na mbili. Pia Kutandaa kunamsaidia kupata taarifa za mafunzo yanayoandaliwa na taasisi nyingine na kushiriki katika mafunzo hayo na matukio mbalimbali ya kinaharakati –forums, matamasha, warsha, mikutano- ndani na nje ya nchi, kwa mfano Januari 2007 alipata bahati ya kuhudhuria tamasha la World Social Forum jijini Nairobi, Kenya.
Baadhi ya harakati anazozikumbuka alizowahi kushiriki kama mwana GDSS ni pamoja na; Mwaka 2006 walitoa msaada kwa binti wa miaka 17 aliyebakwa na mwanamume wa miaka 28, maeneo ya Mabibo MCA ambapo walishirikiana na wananchi kumkamata mbakaji na kumpeleka kituo cha Polisi na kuhakikisha mbakaji amepelekwa mahakamani na mwishoni alifungwa miaka 15.
Ushiriki wa Maandamano ya kumtetea Amina Lawal kuelekea ubalozi wa Nigeria mwaka 2002. Amina alituhumiwa kwa kujamiana nje ya ndoa na kuhukumiwa kifo kwa sharia za kiislamu, kitendo ambacho wanaharakati wote wa haki za binadamu duniani walijitokeza kumtetea, na hatimaye alisamehewa.
Ushiriki wa Maandamano ya kushinikiza mabadiliko ya Sera za IMF na WB dhidi ya Mataifa maskini mwaka 2003 maandamano ambayo yalifanywa kwa lengo la kushinikiza Mataifa ya magharibi kurekebisha sera zao juu ya masoko huria zinazokandamiza nchi maskini.
Kwa kuhitimisha anasema “ushiriki wa semina za kila jumatano unaweza kumbadilisha mtu na mahusiano yake na jamii na kuweza kuleta maendeleo kwa jamii nzima. Wakati umefika sasa kwa wanaharakati kusogeza mikutano kama hii katika maeneo yetu. Vikundi vinaweza kufanya kitu kama hiki katika maeneo yao wanayotoka na kuwezesha kuinua uwezo wa jamii katika utetezi wa rasilimali zao na hivyo kuboresha hali za kimaisha za wananchi. Waandaji kuwaalika wanasiasa wa nchi yetu kuja katika semina hizi na tuweze kuwafahamisha ama kuwaleza maswala tunayohisi kuwa ni ya msingi kwa mustakabali wa nchi na maendeleo ya watu wetu”
Aliwashukuru TGNP kwa kuanda programu hii, na akamalizia kwa kusema, “tunaweza mimi na wewe tukiungana pamoja, Aluta Continua”
5 comments:
ASANTE SANA UONGOZI WA TGNP KWA KUTOA ELIMU YA UELEWA KWA W/HARAKATI. BORA W/HARAKATI NAO WAJIPANGE KUTOA ELIMU HII KWA NCHI NZIMA ILI JAMII IJITAMBUE NI VIPI NA WAPI WANANCHIWATAPATA HAKI ZAO NA KWA NJIA GANI. M/HARAKATI ZAINABU MSANGI HEKIMA GROUP.
ASANTE SANA UONGOZI WA TGNP KWA KUTOA ELIMU YA UELEWA KWA W/HARAKATI. BORA W/HARAKATI NAO WAJIPANGE KUTOA ELIMU HII KWA NCHI NZIMA ILI JAMII IJITAMBUE NI VIPI NA WAPI WANANCHIWATAPATA HAKI ZAO NA KWA NJIA GANI. M/HARAKATI ZAINABU MSANGI HEKIMA GROUP.
ASANTE SANA UONGOZI WA TGNP KWA KUTOA ELIMU YA UELEWA KWA W/HARAKATI. BORA W/HARAKATI NAO WAJIPANGE KUTOA ELIMU HII KWA NCHI NZIMA ILI JAMII IJITAMBUE NI VIPI NA WAPI WANANCHIWATAPATA HAKI ZAO NA KWA NJIA GANI. M/HARAKATI ZAINABU MSANGI HEKIMA GROUP.
Programu hii ni nzuri na itasaidia sana kubadalishana uzoefu baina ya wanaharakati na kuendelea kuwajengea uwezo wanaharakati kwa kupata taarifa kutoka kwa wanaharakati wenzao ni kitu kizuri na kinachopaswa kuendelezwa zaidi.
Suala la kurudisha Rasilimali kwa wananchi si la hiari ni la lazima isipokuwa vipaumbele viwekwe katika kuwawezesha;
-WANANCHI WAZAWA/WAZALENDO
-WANAWAKE
-VIJANA.
By, Hashi S.Luanda,gdss member.
Post a Comment