Sunday, June 15, 2014

BAJETI YA TAIFA 2014/15 JE BAJETI HII NI YA WANANCHI AU YA WAWEKEZAJI?



TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU BAJETI YA TAIFA 2014/15
JE BAJETI HII NI YA WANANCHI  AU YA WAWEKEZAJI?
TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii kutoka maeneno mbali mbali ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS), Kikundi Kazi cha Uchambuzi wa Bajeti (BATT) na Asasi nyingine za Kiraia tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi wa kina na kuanisha maboresho na mapungufu ya  bajeti ya taifa ya 2014/15 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mh. Saada Salum Mkuya tarehe 12 Juni 2014 Bungeni Dodoma.  Kwanza tunaipongeza serikali kwa kuonesha nia madhubuti za kukabiliana na upotevu mkubwa wa mapato kwa kujaribu kurekebisha sheria mbali mbali za kodi. Pia Tunapongeza kuondolewa kwa mamlaka ya waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi, hii ni hatua nzuri ya kuweza kukabiliana na ufisadi, rushwa na watu wachache kunufaika na misamaha ya kodi.
Hata hivyo sehemu kubwa bajeti ya mwaka huu imeonesha mapungufu makubwa katika mfumo mzima wa uwajibikaji wa serikali, katika ukusanyaji wa mapato na hata mgawanyo wake. Lakini pia bajeti hii imeelekezwa zaidi kwa sekta binafsi na wafanyabiashara wakubwa kuliko Watanzania walio wengi ambao ni wazalishaji wadogo na walipa kodi wakubwa.
 Maudhui
Bajeti imeainisha mapato ya shilingi za Kitanzania trilioni 19.9. Kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida ni shilingi trilioni 13.6 (68.3%) wakati shilingi trilioni 6.3 ni matumizi ya maendeleo sawa na (31.7%). Tumeshtushwa kuona bajeti ya maendeleo haijaongezeka kama tulivyorajia. wakati kwa sehemu kubwa ndio tegemeo kwa maendeleo ya Watanzania.  Tunasikitika kwasababu hakuna tofauti kubwa kati ya bajeti ya mwaka jana wa fedha 2013/2014 ambayo matumizi ya kawaida yalikuwa Trilioni 12.6 (69.2%) na matumizi ya maendeleo Trilioni 5.6 (30.8%).
Deni la Taifa
Tumeshangazwa kuona deni la taifa likiongezeka kufikia  shilingi za Kitanzania trilioni  30.5 ukilinganisha na Trilioni 23.6 mwezi Machi 2013, na kuwa kubwa kuliko bajeti ya taifa huku serikali ikisema kuwa deni hili ni himilivu. Licha ya kwamba deni hili la taifa linazidi kukua, bado tunashangaa kuona serikali inasisitiza kuendelea kukopa kwa kigezo cha deni kuwa himilivu na kwamba serikali inakopesheka. Wakati huohuo Serikali inashindwa kusimamia ulinzi na mgawanyo mzuri wa rasilimali tulizo nazo na inatoa misamaha ya kodi isio na tija kwa taifa.. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kiasi cha shilingi trilioni 1.6 kilipotea kutokana na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija. Tunadai uwajibikaji wa serikali katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ambavyo ni endelevu.

Vipaumbele vya Bajeti
Serikali imeweka vipaumbele zaidi katika sekta ambazo zipo katika mpango wa Matokeo makubwa sasa (Maji, Kilimo, Elimu, utawala bora na miundo mbinu). Sekta hizi zimetengewa kiasi cha Trilioni 7.9.  Tunadai pia uendelevu wa sekta nyingine kama Afya ambayo imekua na matatizo makubwa hasa kwenye eneo la afya ya uzazi na afya ya jamii. Tunahoji sekta ya afya kutokua sehemu ya  vipaumbele  hivi  wakati wanawake na watoto hawana uhakika na upatikanaji wa huduma za afya nchini na wanawake takribani 24 kufa kila siku kwa uzazi.
Pamoja na kupongeza kuondolewa kwa mamlaka ya waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi tuna mashaka na ongezeko kubwa la misamaha ya kodi kwa mapato yasiokuwa na mauzo ya hatifungani kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) katika soko la mitaji ya Tanzania ambalo wakopaji wake ni wawekezaji wakubwa, huku wafanyabiashara wadogo wenye kipato kati ya milioni 4 hadi milioni 7 kwa mwaka  wakiongezewa mzigo mkubwa wa ulipaji kodi. Sekta isio rasmi haikuwekewa mazingira mazuri ya ukuaji na wakopaji wakubwa ni Wanawake, Vijana na wanaume maskini. Tunadai uwepo wa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo pamoja na mfumo mzuri wa sekta isiyo rasmi ambayo kwa sehemu kubwa ndio kimbilio la wanyonge.
Katika sekta ya kilimo mkazo umewekwa katika kutoa misamaha ya kodi kwenye Matrekta ambayo yataendelea kuagizwa nchini bila ya kulipiwa ushuru. Msamaha huu wa kodi haujatengeza mazingira ya namna ya kumnufaisha mkulima mdogo nchini na badala yake unanufaisha wakulima wakubwa na wakodishaji wa matrekta hayo. Jambo hili linaendeleza mfumo wa unyonyaji na ubepari  kwa wakulima wadogo na kupanua wigo wa matabaka kati ya wakulima wadogo na wakubwa. Pia  mpango huu unaendeleza ulimbikizaji kiporaji wa ardhi nchini na kuongeza migogoro isiyoisha kati ya wawekezaji na wakulima wadogo, na wafugaji. Tunadai mgawanyo wa ardhi uendane na mahitaji ya makundi katika maeneo husika hususani kwa wanawake, vijana na wanaume maskini.
Serikali imeonesha juhudi za makusudi za kutaka kulinda viwanda na bidhaa za ndani kwa kuongeza kodi kwa bidhaa ambazo zinaagizwa kutoka nje ya nchi. Tunashauri mkakati huo huo ufanywe pia ili kuwalinda wawekezaji wadogo wanaowekeza kwenye gesi asilia pamoja na mafuta. Hii itasaidia kuongeza tija kwa wawekezaji wadogo katika uchimbaji pamoja na uvunaji na hatimae itasaidia kuinua pato la taifa na kupunguza utegemezi wa kibajeti nchini.
Katika hotuba ya bajeti serikali imesema imetoa jumla ya ajira mpya 630,616 kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na idadi ya wahitimu 900,000 wanaoingia kwenye soko la  ajira kila mwaka pamoja na wale waliopo tayari. Tunahoji ajira hizi zilizotolewa na serikali kwa mwaka 2013/2014 zinakidhi mahitaji ya soko la ajira? Na Je ajira hizi ni salama na endelevu zinazojali utu, heshima na staha? Bado tunadai mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa malighafi vikubwa na vidogo vinavyoweza kuongeza ajira kwa waliokuwa wengi vijijini na mijini.
Katika sekta ya  elimu serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni  500 kwa ajili ya halmashauri 80  kujenga nyumba za walimu. Kiasi kama hiki kilitengwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa halmashauri 40 nchini. Tunahoji pesa hizo zilizotumika zilijenga nyumba ngapi na katika halmashauri zipi na zenye ubora gani? Je upo wapi mkakati wa ujenzi wa mabweni, kuboresha mazingira ya kufundishia na vifaa vya kujifunzia, na mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu?
Mwisho tumesikitishwa sana kuona Waziri wa Fedha akikiri bungeni kwamba sera zetu za kiuchumi zinatokana na mashirika makubwa ya kibeberu kama vile IMF kupitia mpango wa  Policy Support Instrument (PSI). Hali hii inathibitisha kwamba mipango mingi iliyopo nchini haitokani na wananchi bali matakwa ya mashirika makubwa yanayoendeleza ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali nchini. Lakini pia serikali inaendelea  kupuuza utaalamu wa wataalamu wa uchumi wa ndani ya nchi.

Madai
Kutokana na uchambuzi ulioainishwa hapo juu tunadai yafuatayo:
  1. Kuwepo mfumo shirikishi na endelevu katika kutengeneza na kufatilia utekelezaji wa bajeti ya taifa na serikali za mitaa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi, wanawake na wanaume na makundi yaliyoko pembezoniMisamaha ya kodi katika kilimo ilenge kuwanufaisha wakulima wadogo wadogo na sio wawekezaji wakubwa.
  2. Kukua kwa uchumi wa nchi kuende  sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote  wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
  3. Sekta ya afya ipewe kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kuhakikisha bajeti inafikia 15% ya bajeti ya taifa kama ilivyoagizwa katika azimio la Abuja.
  4. Uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji  na usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa na tija.

Tamko hili limetolewa na:
Sisi wanaharakati wa kikundi kazi cha uchambuzi wa bajeti,  wanaharakati kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS),kwa ushirikiano na TGNP Mtandao

Imesainiwa na:

Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao

Tarehe 15 Juni 2014   

No comments: