TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU BAJETI YA TAIFA 2014/15
JE BAJETI HII NI YA WANANCHI AU YA WAWEKEZAJI?
TGNP Mtandao kwa kushirikiana
na wanaharakati ngazi ya jamii kutoka maeneno mbali mbali ya Dar es Salaam,
Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo
(GDSS), Kikundi Kazi cha Uchambuzi wa Bajeti (BATT) na Asasi nyingine za Kiraia
tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi wa kina na kuanisha maboresho na
mapungufu ya bajeti ya taifa ya 2014/15
iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mh. Saada Salum Mkuya tarehe 12 Juni
2014 Bungeni Dodoma. Kwanza tunaipongeza
serikali kwa kuonesha nia madhubuti za kukabiliana na upotevu mkubwa wa mapato
kwa kujaribu kurekebisha sheria mbali mbali za kodi. Pia Tunapongeza kuondolewa
kwa mamlaka ya waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi, hii ni hatua nzuri ya
kuweza kukabiliana na ufisadi, rushwa na watu wachache kunufaika na misamaha ya
kodi.
Hata hivyo sehemu kubwa bajeti
ya mwaka huu imeonesha mapungufu makubwa katika mfumo mzima wa uwajibikaji wa
serikali, katika ukusanyaji wa mapato na hata mgawanyo wake. Lakini pia bajeti
hii imeelekezwa zaidi kwa sekta binafsi na wafanyabiashara wakubwa kuliko
Watanzania walio wengi ambao ni wazalishaji wadogo na walipa kodi wakubwa.
Maudhui
Bajeti
imeainisha mapato ya shilingi za Kitanzania trilioni 19.9. Kati ya fedha hizo
matumizi ya kawaida ni shilingi trilioni 13.6 (68.3%) wakati shilingi trilioni
6.3 ni matumizi ya maendeleo sawa na (31.7%). Tumeshtushwa kuona bajeti ya
maendeleo haijaongezeka kama tulivyorajia. wakati kwa sehemu kubwa ndio tegemeo
kwa maendeleo ya Watanzania.
Tunasikitika kwasababu hakuna tofauti kubwa kati ya bajeti ya mwaka jana
wa fedha 2013/2014 ambayo matumizi ya kawaida yalikuwa Trilioni 12.6 (69.2%) na
matumizi ya maendeleo Trilioni 5.6 (30.8%).
Deni la Taifa
Tumeshangazwa
kuona deni la taifa likiongezeka kufikia shilingi za Kitanzania trilioni 30.5 ukilinganisha na Trilioni 23.6 mwezi Machi
2013, na kuwa kubwa kuliko bajeti ya taifa huku serikali ikisema kuwa deni hili
ni himilivu. Licha ya kwamba deni
hili la taifa linazidi kukua, bado tunashangaa kuona serikali inasisitiza
kuendelea kukopa kwa kigezo cha deni kuwa himilivu na kwamba serikali
inakopesheka. Wakati huohuo Serikali inashindwa kusimamia ulinzi na mgawanyo
mzuri wa rasilimali tulizo nazo na inatoa misamaha ya kodi isio na tija kwa
taifa.. Kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kiasi cha shilingi trilioni 1.6
kilipotea kutokana na misamaha ya kodi isiyokuwa na tija. Tunadai uwajibikaji wa serikali katika kusimamia ukusanyaji wa mapato
na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ambavyo ni endelevu.
Vipaumbele vya
Bajeti
Serikali
imeweka vipaumbele zaidi katika sekta ambazo zipo katika mpango wa Matokeo
makubwa sasa (Maji, Kilimo, Elimu, utawala bora na miundo mbinu). Sekta hizi
zimetengewa kiasi cha Trilioni 7.9. Tunadai
pia uendelevu wa sekta nyingine kama Afya ambayo imekua na matatizo makubwa
hasa kwenye eneo la afya ya uzazi na afya ya jamii. Tunahoji sekta ya afya
kutokua sehemu ya vipaumbele hivi
wakati wanawake na watoto hawana uhakika na upatikanaji wa huduma za afya
nchini na wanawake takribani 24 kufa kila siku kwa uzazi.
Pamoja
na kupongeza kuondolewa kwa mamlaka ya waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi
tuna mashaka na ongezeko kubwa la misamaha ya kodi kwa mapato yasiokuwa na
mauzo ya hatifungani kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) katika soko la
mitaji ya Tanzania ambalo wakopaji wake ni wawekezaji wakubwa, huku
wafanyabiashara wadogo wenye kipato kati ya milioni 4 hadi milioni 7 kwa
mwaka wakiongezewa mzigo mkubwa wa
ulipaji kodi. Sekta isio rasmi haikuwekewa mazingira mazuri ya ukuaji na
wakopaji wakubwa ni Wanawake, Vijana na wanaume maskini. Tunadai uwepo wa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo pamoja na
mfumo mzuri wa sekta isiyo rasmi ambayo kwa sehemu kubwa ndio kimbilio la
wanyonge.
Katika
sekta ya kilimo mkazo umewekwa katika kutoa misamaha ya kodi kwenye Matrekta
ambayo yataendelea kuagizwa nchini bila ya kulipiwa ushuru. Msamaha huu wa kodi
haujatengeza mazingira ya namna ya kumnufaisha mkulima mdogo nchini na badala
yake unanufaisha wakulima wakubwa na wakodishaji wa matrekta hayo. Jambo hili
linaendeleza mfumo wa unyonyaji na ubepari
kwa wakulima wadogo na kupanua wigo wa matabaka kati ya wakulima wadogo
na wakubwa. Pia mpango huu unaendeleza
ulimbikizaji kiporaji wa ardhi nchini na kuongeza migogoro isiyoisha kati ya
wawekezaji na wakulima wadogo, na wafugaji. Tunadai mgawanyo wa ardhi uendane na mahitaji ya makundi katika maeneo husika
hususani kwa wanawake, vijana na wanaume maskini.
Serikali
imeonesha juhudi za makusudi za kutaka kulinda viwanda na bidhaa za ndani kwa
kuongeza kodi kwa bidhaa ambazo zinaagizwa kutoka nje ya nchi. Tunashauri mkakati
huo huo ufanywe pia ili kuwalinda wawekezaji wadogo wanaowekeza kwenye gesi
asilia pamoja na mafuta. Hii itasaidia kuongeza tija kwa wawekezaji wadogo
katika uchimbaji pamoja na uvunaji na hatimae itasaidia kuinua pato la taifa na
kupunguza utegemezi wa kibajeti nchini.
Katika hotuba ya bajeti serikali
imesema imetoa jumla ya ajira mpya 630,616 kiwango hiki ni kidogo sana
ukilinganisha na idadi ya wahitimu 900,000 wanaoingia kwenye soko la
ajira kila mwaka pamoja na wale waliopo tayari. Tunahoji ajira hizi
zilizotolewa na serikali kwa mwaka 2013/2014 zinakidhi mahitaji ya soko la
ajira? Na Je ajira
hizi ni salama na endelevu zinazojali utu, heshima na staha? Bado tunadai
mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa malighafi vikubwa
na vidogo vinavyoweza kuongeza ajira kwa waliokuwa wengi vijijini na mijini.
Katika sekta ya elimu serikali imetenga kiasi cha Shilingi
Milioni 500 kwa ajili ya halmashauri 80 kujenga nyumba za walimu. Kiasi kama hiki
kilitengwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa halmashauri 40 nchini. Tunahoji
pesa hizo zilizotumika zilijenga nyumba ngapi na katika halmashauri zipi na
zenye ubora gani? Je upo wapi mkakati wa ujenzi wa mabweni, kuboresha mazingira
ya kufundishia na vifaa vya kujifunzia, na mazingira wezeshi kwa watu wenye
ulemavu?
Mwisho tumesikitishwa sana
kuona Waziri wa Fedha akikiri bungeni kwamba sera zetu za kiuchumi zinatokana
na mashirika makubwa ya kibeberu kama vile IMF kupitia mpango wa Policy Support Instrument (PSI). Hali hii
inathibitisha kwamba mipango mingi iliyopo nchini haitokani na wananchi bali
matakwa ya mashirika makubwa yanayoendeleza ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali
nchini. Lakini pia serikali inaendelea kupuuza utaalamu wa wataalamu wa uchumi wa ndani
ya nchi.
Madai
Kutokana na uchambuzi
ulioainishwa hapo juu tunadai yafuatayo:
- Kuwepo mfumo shirikishi na endelevu katika kutengeneza na kufatilia utekelezaji wa bajeti ya taifa na serikali za mitaa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi, wanawake na wanaume na makundi yaliyoko pembezoniMisamaha ya kodi katika kilimo ilenge kuwanufaisha wakulima wadogo wadogo na sio wawekezaji wakubwa.
- Kukua kwa uchumi wa nchi kuende sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
- Sekta ya afya ipewe kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kuhakikisha bajeti inafikia 15% ya bajeti ya taifa kama ilivyoagizwa katika azimio la Abuja.
- Uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa na tija.
Tamko hili limetolewa na:
Sisi
wanaharakati wa kikundi kazi cha uchambuzi wa bajeti, wanaharakati kutoka Dar es Salaam, Mbeya,
Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo
(GDSS),kwa ushirikiano na TGNP Mtandao
Imesainiwa na:
Lilian Liundi
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao
Tarehe 15 Juni 2014