Monday, October 21, 2013

TGNP na juhudi za ukombozi wa kijinsia Tanzania






MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni taasisi huru inayotoa chachu ya ujenzi wa tapo la harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi nchini Tanzania, barani Afrika na kwingineko duniani.

Mtandao ulianzishwa wakati kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani na nchini Tanzania kati ya miaka ya 1980 na1990.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa TGNP, Usu Mallya, mabadiliko hayo yalitoa msukumo mkubwa wa kuanzishwa kwake na kipindi hiki kilitawaliwa na mikakati ya maendeleo iliyoongozwa na Benki ya Dunia (World Bank) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IMF) katika kurekebisha uchumi.

Mallya alisema hayo hivi karibuni katikia Tamasha la 11 la Jinsia 2013 lililofanyika katika viwanja vya TGNP vilivyopo Mabibo Septemba 3 hadi 6, mwaka huu na kusisitiza kuwa malengo makuu ya urekebishaji huu yalikuwa kulegeza masharti ya biashara na kupunguza nafasi ya Serikali katika kusimamia uchumi na rasilimali za taifa.

Mallay alisema malengo mengine “Ni kuweka kipaumbele kwa uwezeshaji wa sekta binafsi ; kuondokana na siasa na itikadi ya ujamaa na kujitegemea na kasumba ya kukumbatia upepari na uliberali mamboleo.”

Anasema, “Mabadiliko haya yalikuwa na taathira nyingi hasi nchini zikiwemo kupunguza wafanyakazi hasa kwenye mashirika ya umma; kukosa uhakika wa ajira kwa wengi wakiwamo wanawake, pamoja na rasilimali za umma zilizojengwa kwa jasho la wengi kuchukuliwa na wachache wengi wakiwa wageni na makampuni makubwa ya kibepari, hivyo kujengeka kwa kasi kwa tabaka na wenye nacho na wasio nacho.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TGNP anasema athari nyingine zilikuwa majukumu  ya huduma za kijamii kurudishwa katika ngazi ya familia mzigo ambao umeendelea kubebwa na wanawake kwa kiwango kikubwa hadi sasa.

“Hadi leo kulikuwepo na adhari nyingi zilizowakuta wananchi maskini wakiwemo wanaume na hasa wanawake, athari hizi zilijumuisha kukosekana kwa huduma muhimu kama afya/afya ya uzazi, elimu na mengine kutokana na sera zinazoelekeza kuwa serikali kupunguza nguvu ya kuwekeza kwenye sekta kama afya na elimu tofauti kubwa zimeendelea kujengeka kati ya miji na vijiji, kimikoa, kikanda, kiumri, wenye ulemavu wenye kuishi na VVU/Ukimwi na tofauti nyingine zote.”

MATOKEO YAKE NI NINI?

Mkurugenzi huyo nasema, “Tunaendelea leo kuona athari nyingi hususan katika kuporomoka kwa dhana ya uwajibikaji kwa jamii, ufisadi na rushwa zilizokithiri, kuzorota kwa ufikiaji na ubora wa huduma mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, afya na nishati,”
Kadhalika, “Kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kukua kwa uchumi bila ajira, na uporaji mkubwa wa ardhi, madini, maji, gesi, na rasilimali nyinginezo.”

Anasema kwa mantiki hii “Kuanzia mwanzo Mtandao ulijengwa katika misingi ya kupambana na mfumo wa uliberali mamboleo (yaani utandawazi wizi) na mfumo dume ambayo ndiyo kiini cha tofauti za kijinsia kati ya wanawake na wanaume na  kusukuma makundi mengi pembezoni.”

Uchunguzi wa makala yaha umebaini kuwa, muktadha huu wa ujenzi wa kitabaka, uliojengeka katika mifumo mingine kandamizi ikiwemo mfumo dume, fursa ya kuanzishwa kwa Mtandao iliyoelekeza wakati wa  maandalizi ya wanawake wa  Tanzania kushiriki , Mkutano wa Beijing mwaka 1995.

Semina tatu za maandalizi ziliongozwa na timu ya wanaharakati. Dhana ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi na mbinu za uraghbishi katika kuibua masuala na wanawake na kuyaainisha katika muktadha wa soko huria na mfumo dume ulitoa hamasa ya kipekee na Madai ya umuhimu wa kuanzishwa kwa taasisi itakayoendeleza kutandaa na kupashana habari kuhusu masuala ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia na haki ya jamii nchini.

Ndipo Mtandao wa Jinsia ukaandikishwa rasmi mwaka 1993 kama shirika lisilo la kiserikali lenye   dira ambayo ni kuona jamii ya kitanzania inayojali na kuhakikisha haki za wanawake, usawa wa kijinsia na haki za kijamii.

DHIMA NA DHAMIRA YA TGNP

 Katika mada iliyotolewa kwa ushirikiano na Profesa Marjorie Mbilinyi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Mary Rusimbi isemayo “MIAKA 20 YA HARAKATI ZA UKOMBOZI WA WANAWAKE NCHINI TANZANIA: TUKO WAPI NA TUNAKWENDA WAPI?”  Mallya anasema, “Mabadiliko tunayotaka katika mifumo kandamizi na sera zake hayawezi kutokana na vitendo vya mtu mmoja wala taasisi au kikundi kimoja pekee, bali tunahitaji kujenga nguvu za pamoja.”

“Kwa kutumia dhana na nadharia ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika misingi uraghbishi na UTATU yaani Utambuzi, Uchambuzi, Utatuzi/Utekelezaji, TGNP Mtandao umetoa mchango wa kipekee nchini Tanzania, barani Afrika na kwingineko duniani.”

Mkurugenzi huyo anajivunia mafanikio ya TGNP akisema, “Taasisi hii pia imetukuka katika kuwa na msimamo usiotikisika kuhusu umuhimu wa kubomoa mifumo yote kandamizi ili kufikia maendelo endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.”

Anafahamisha akisema, “Msingi wa dhana ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi ni mahusiano ya kijinsia na tabaka, hatutenganishi, bali tunaunga masuala haya kwa maana nia yetu ni kubomoa mifumo ya ubepari na ubeberu na kwa maneno mengine, utandawazi wizi na mfumo dume.”

NAMNA YA KUIBOMOA MIFUMO KANDAMIZI

TGNP inasema, “Dhana ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi inatuongoza jinsi taasisi yetu inavyofanya kazi, mfumo wake wa uongozi shirikishi, mipango yetu ya utafiti shirikishi na wanaharakati wa ngazi ya jamii, jinsi tunavyounganisha utafiti shirikishi na vyombo vya habari ili kuwezesha madai ya wananchi yawafikie wengi pamoja na  viongozi wa serikali za mitaa na serikali kuu.”

Mallya anasema kuwa, mchakato huu ni fursa ya wanajamii kukutana, kutafakari, kutafuta taarifa mbalimbali na kujenga nguvu za pamoja katika kudai haki na fursa sawa kwa rasilimali zote yaani ardhi, madini, gesi, maji, fedha/bajeti, ajira, taarifa pamoja na uwajibikaji wa huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu, maji, malezi, malazi, nishati, usafiri na hasa, na kukataa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

MTANDAO ULIPO SASA
TGNP inasema muktadha wa sasa hauna tofauti kubwa na ule wa miaka 20 iliyopita kwani azma ya awali ya soko huria, upepari na uliberali mamboleo bado uko pale pale. 

“Kilichobadilika ni kuongezeka kwa kasi kwa utekelezaji wa azma hiyo hususan kutokana na mtikisiko wa uchumi duniani hasa kuanzia 2008, kuporomoka kwa mfumo wa fedha na mtikisiko wa mfumo mzima wa ubepari wa kibwanyenye duniani,” anasema Mallya.

Anaongeza, “Matokeo yake ni  zahma mpya za kiuchumi ambapo tunashuhudia  mbinu za wazi na za kikatili zaidi za kutekeleza azma hiyo zikiwemo uporaji wa wazi wa maliasili, ardhi, madini, gesi na maji.”

Kwa mujibu wa TGNP,  kumekuwa na badiliko ya kisera kutoka kwa nchi wahisani  toka mwelekeo walau kidogo wa kushughulikia masuala ya umaskini na kuendeleza uwekezaji na biashara kama msingi mkuu wa kuleta maendeleo, bila kusahau uwekezaji mwingi ni wa makampuni kutaka nchi iwape maeneo yao.”
NINI KIMEFANYIKA?
Mtandao wa Jinsia umetoa mchango mkubwa katika michakato mbalimbali ikiwa na malengo ya kutoa fursa za kuhoji/kutafakari, kujenga nguvu za pamoja katika ngazi ya taifa, kikanda na kimataifa.yanayojitokeza  hapo chini  ni kati ya yale mengi yaliyotekelezwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Kadhalika, Muungano wa Taasis takribani 50 zinazotetea haki za binadamu,demokrasia na maendeleo (Fem Act) katika ngazi ya kitaifa ilianzishwa kama jukwaa lenye mrengo wa harakati za ukombozi wa wanawake linalounganisha mashirika yanayotetea haki za binadamu, harakati za rasilimali, utawala bora na demokrasia, haki za huduma za jamii.

Kutambua nguvu ya kila taasisi na kutoa sauti na kujenga nguvu za pamoja katika masuala mbalimbali ya mstakabali wa Taifa, uongozi, ufisadi, harakati za Sheria ya Makosa ya Kujamiina (SOSPA), iliyoongozwa na TAMWA, na sheria ya Ardhi .

“Mtandao wa Jinsia kutoa mchango katika mapambano mapana mfano ya ardhi na ya kuhakikisha suala la jinsia linapewa kipaumbele katika mchakato mzima; ndivyo hivyo hata katika mchakato wa sasa wa Katiba,” anasema Mallya.
                                                
Katika kipindi hiki TGNP inasema, imeendelea kujitahidi kutoa sauti na msimamo katika kuzungumzia maeneo yenye ukimya ikiwemo mfumo dume na mwingiliano wake na mfumo wa kiliberali mamboleo; pamoja na soko huria; suala la UKIMWI na VVU kuwa ni la rasilimali na jinsia.

“Ndio maana tunatumia fursa mbalimbali kuvunja ukimya kuhusu suala la rushwa ya ngono, tukihusisha masuala ya mifumo ya kugawa rasilimali inayowapa  wachache nafasi zaidi, huku ikipokonya uwezo wa wengi kujipatia ajira endelevu na zenye hadhi wengi kukosa huduma,” Mallya anasema.

Anaongeza, “Hiki ndicho kiini kinachozaa rushwa ya ngono kwa mfano, wanafunzi kutokana na ufinyu wa mabweni ya kutosha wanafunzi hutozwa hela wakati wa kutaka vyumba kwenye vyuo na wanafunzi wa kike kudaiwa rushwa ya ngono.”

Mtandao huo kwa mujibu wa Mallya, unasema lengo hasa ni kudai rushwa ya ngono ili izungumzwe kama sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini Tanzania, uwajibikaji kuhusu rushwa ya ngono hususan kupitia kamati za maadili katika taasisi serikalini, sekta binafsi na nyingine zote ambazo hatuoni zikielekeza nguvu katika suala hili.

“Lingine ni kuanzishwa kwa bajeti ya kijinsia kama nyenzo ya kudai na kuelekeza rasilimali fedha katika kushughulikia haki za wanawake na usawa wa kijinsia. Hii ni nyenzo ya wanaharakati kudai uwajibikaji, kupata taarifa za mapato na matumizi na kufuatilia bajeti katika ngazi ya taifa, sekta na serikali za mitaa.”

KURASIMISHA HARAKATI ZA UKOMBOZI WA WANAWAKE KIMAPINDUZI
Ili kuhakikisha kwa itikadi na dhamira ya TGNP Mtandao inakuwa endelevu, jitihada kubwa zilifanyika tangu mwanzo kurasimisha misingi ya harakati hizi katika Sera, mipango, utaratibu wa utendaji kazi, uwajibikaji wa pamoja na kwa binafsi na zaidi ya yote katika uongozi wa TGNP Mtandao.
KUNA CHANGAMOTO GANI?
Changamoto zilizopo ni pamoja na kuendelea kuzungukwa na muktadha kimfumo, kisera, kisiasa na kuitamaduni unaoendeleza itikadi ya ubabe, kuendeleza kwa kasi kwa nadharia ya uzuri wa soko huria wakati upo msimamo wa kuwawezesha wanyonge na hususan wanawake walioko pembezoni kunufaika zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TGNP anasema, “Muktadha huu unaongeza nafasi ya kukua kwa mfumo dume katika ngazi zote na kupunguza fursa za wanaharakati kuleta mabadiliko ya kweli.”

Anasema, “Kwa mfano, kujengeka kwa tabaka, kuwa wabinafsi zaidi kila mmoja akijaribu kujitafutia fursa mwenyewe na familia yake, kushusha maonevu kati ya sisi kwa sisi na kuanza kupigana wenyewe kwa mfano wafugaji na wakulima wadogo wadogo kuchinjana badala ya kutambua adui mkubwa na kutokutumia fursa za kujenga nguvu za pamoja kumkabili adui.”

“Kukosekana kwa ajira endelevu, na kipato cha uhakika na kurudisha majukumu nyumbani kumepelekea hasira na kuendelea kwa ukatili dhidi ya wanawake hususan kutoka kwa waume au wapenzi wao.”

No comments: