MTANDAO wa Jinsia
Tanzania (TGNP) ni taasisi huru inayotoa chachu ya ujenzi wa tapo la harakati
za ukombozi wa wanawake kimapinduzi nchini Tanzania, barani Afrika na
kwingineko duniani.
Mtandao ulianzishwa
wakati kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani na nchini Tanzania kati ya
miaka ya 1980 na1990.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
wa TGNP, Usu Mallya, mabadiliko hayo yalitoa msukumo mkubwa wa kuanzishwa kwake
na kipindi hiki kilitawaliwa na mikakati ya maendeleo iliyoongozwa na Benki ya
Dunia (World Bank) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IMF) katika kurekebisha
uchumi.
Mallya alisema
hayo hivi karibuni katikia Tamasha la 11 la Jinsia 2013 lililofanyika katika
viwanja vya TGNP vilivyopo Mabibo Septemba 3 hadi 6, mwaka huu na kusisitiza
kuwa malengo makuu ya
urekebishaji huu yalikuwa kulegeza masharti ya biashara na kupunguza nafasi ya
Serikali katika kusimamia uchumi na rasilimali za taifa.
Mallay alisema malengo mengine “Ni kuweka
kipaumbele kwa uwezeshaji wa sekta binafsi ; kuondokana na siasa na itikadi ya
ujamaa na kujitegemea na kasumba ya kukumbatia upepari na uliberali mamboleo.”
Anasema, “Mabadiliko
haya yalikuwa na taathira nyingi hasi nchini zikiwemo kupunguza wafanyakazi
hasa kwenye mashirika ya umma; kukosa uhakika wa ajira kwa wengi wakiwamo
wanawake, pamoja na rasilimali za umma zilizojengwa kwa jasho la wengi
kuchukuliwa na wachache wengi wakiwa wageni na makampuni makubwa ya kibepari,
hivyo kujengeka kwa kasi kwa tabaka na wenye nacho na wasio nacho.”
Mkurugenzi Mtendaji huyo
wa TGNP anasema athari nyingine zilikuwa majukumu ya huduma za kijamii kurudishwa katika ngazi
ya familia mzigo ambao umeendelea kubebwa na wanawake kwa kiwango kikubwa hadi
sasa.
“Hadi leo kulikuwepo na
adhari nyingi zilizowakuta wananchi maskini wakiwemo wanaume na hasa wanawake,
athari hizi zilijumuisha kukosekana kwa huduma muhimu kama afya/afya ya uzazi,
elimu na mengine kutokana na sera zinazoelekeza kuwa serikali kupunguza nguvu
ya kuwekeza kwenye sekta kama afya na elimu tofauti kubwa zimeendelea kujengeka
kati ya miji na vijiji, kimikoa, kikanda, kiumri, wenye ulemavu wenye kuishi na
VVU/Ukimwi na tofauti nyingine zote.”
MATOKEO YAKE NI NINI?
Mkurugenzi huyo nasema, “Tunaendelea
leo kuona athari nyingi hususan katika kuporomoka kwa dhana ya uwajibikaji kwa
jamii, ufisadi na rushwa zilizokithiri, kuzorota kwa ufikiaji na ubora wa
huduma mbalimbali zikiwemo za maji, elimu, afya na nishati,”
Kadhalika, “Kuongezeka
kwa ukatili dhidi ya wanawake na watoto, kukua kwa uchumi bila ajira, na
uporaji mkubwa wa ardhi, madini, maji, gesi, na rasilimali nyinginezo.”
Anasema kwa mantiki hii
“Kuanzia mwanzo Mtandao ulijengwa katika misingi ya kupambana na mfumo wa
uliberali mamboleo (yaani utandawazi wizi) na mfumo dume ambayo ndiyo kiini cha
tofauti za kijinsia kati ya wanawake na wanaume na kusukuma makundi mengi pembezoni.”
Uchunguzi wa makala yaha
umebaini kuwa, muktadha huu wa ujenzi wa kitabaka, uliojengeka katika mifumo mingine
kandamizi ikiwemo mfumo dume, fursa ya kuanzishwa kwa Mtandao iliyoelekeza
wakati wa maandalizi ya wanawake wa Tanzania kushiriki , Mkutano wa Beijing mwaka
1995.
Semina tatu za maandalizi
ziliongozwa na timu ya wanaharakati. Dhana ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi
na mbinu za uraghbishi katika kuibua masuala na wanawake na kuyaainisha katika
muktadha wa soko huria na mfumo dume ulitoa hamasa ya kipekee na Madai ya
umuhimu wa kuanzishwa kwa taasisi itakayoendeleza kutandaa na kupashana habari
kuhusu masuala ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia na haki ya jamii
nchini.
Ndipo Mtandao wa Jinsia
ukaandikishwa rasmi mwaka 1993 kama shirika lisilo la kiserikali lenye dira ambayo ni kuona jamii ya kitanzania
inayojali na kuhakikisha haki za wanawake, usawa wa kijinsia na haki za
kijamii.
DHIMA NA DHAMIRA YA TGNP
Katika mada iliyotolewa kwa ushirikiano na Profesa
Marjorie Mbilinyi pamoja na Mwenyekiti
wa Bodi ya TGNP, Mary Rusimbi isemayo “MIAKA 20 YA HARAKATI ZA UKOMBOZI WA
WANAWAKE NCHINI TANZANIA: TUKO WAPI NA TUNAKWENDA WAPI?” Mallya anasema, “Mabadiliko
tunayotaka katika mifumo kandamizi na sera zake hayawezi kutokana na vitendo
vya mtu mmoja wala taasisi au kikundi kimoja pekee, bali tunahitaji kujenga nguvu
za pamoja.”
“Kwa kutumia dhana na
nadharia ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika misingi uraghbishi na UTATU
yaani Utambuzi, Uchambuzi, Utatuzi/Utekelezaji, TGNP Mtandao umetoa mchango wa
kipekee nchini Tanzania, barani Afrika na kwingineko duniani.”
Mkurugenzi huyo
anajivunia mafanikio ya TGNP akisema, “Taasisi hii pia imetukuka katika kuwa na
msimamo usiotikisika kuhusu umuhimu wa kubomoa mifumo yote kandamizi ili
kufikia maendelo endelevu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.”
Anafahamisha akisema,
“Msingi wa dhana ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi ni mahusiano ya kijinsia
na tabaka, hatutenganishi, bali tunaunga masuala haya kwa maana nia yetu ni
kubomoa mifumo ya ubepari na ubeberu na kwa maneno mengine, utandawazi wizi na
mfumo dume.”
NAMNA YA KUIBOMOA MIFUMO KANDAMIZI
TGNP inasema, “Dhana ya
ukombozi wa wanawake kimapinduzi inatuongoza jinsi taasisi yetu inavyofanya
kazi, mfumo wake wa uongozi shirikishi, mipango yetu ya utafiti shirikishi na
wanaharakati wa ngazi ya jamii, jinsi tunavyounganisha utafiti shirikishi na
vyombo vya habari ili kuwezesha madai ya wananchi yawafikie wengi pamoja
na viongozi wa serikali za mitaa na
serikali kuu.”
Mallya anasema kuwa,
mchakato huu ni fursa ya wanajamii kukutana, kutafakari, kutafuta taarifa
mbalimbali na kujenga nguvu za pamoja katika kudai haki na fursa sawa kwa
rasilimali zote yaani ardhi, madini, gesi, maji, fedha/bajeti, ajira, taarifa
pamoja na uwajibikaji wa huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu, maji,
malezi, malazi, nishati, usafiri na hasa, na kukataa ukatili dhidi ya wanawake
na watoto.
MTANDAO ULIPO SASA
TGNP inasema muktadha wa
sasa hauna tofauti kubwa na ule wa miaka 20 iliyopita kwani azma ya awali ya
soko huria, upepari na uliberali mamboleo bado uko pale pale.
“Kilichobadilika ni
kuongezeka kwa kasi kwa utekelezaji wa azma hiyo hususan kutokana na mtikisiko
wa uchumi duniani hasa kuanzia 2008, kuporomoka kwa mfumo wa fedha na mtikisiko
wa mfumo mzima wa ubepari wa kibwanyenye duniani,” anasema Mallya.
Anaongeza, “Matokeo yake
ni zahma mpya za kiuchumi ambapo
tunashuhudia mbinu za wazi na za
kikatili zaidi za kutekeleza azma hiyo zikiwemo uporaji wa wazi wa maliasili,
ardhi, madini, gesi na maji.”
Kwa mujibu wa TGNP, kumekuwa na badiliko ya kisera kutoka kwa
nchi wahisani toka mwelekeo walau kidogo
wa kushughulikia masuala ya umaskini na kuendeleza uwekezaji na biashara kama
msingi mkuu wa kuleta maendeleo, bila kusahau uwekezaji mwingi ni wa makampuni
kutaka nchi iwape maeneo yao.”
NINI KIMEFANYIKA?
Mtandao wa Jinsia umetoa
mchango mkubwa katika michakato mbalimbali ikiwa na malengo ya kutoa fursa za
kuhoji/kutafakari, kujenga nguvu za pamoja katika ngazi ya taifa, kikanda na
kimataifa.yanayojitokeza hapo chini ni kati ya yale mengi yaliyotekelezwa katika
kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Kadhalika, Muungano wa Taasis takribani 50 zinazotetea haki za
binadamu,demokrasia na maendeleo (Fem Act) katika ngazi ya kitaifa ilianzishwa kama
jukwaa lenye mrengo wa harakati za ukombozi wa wanawake linalounganisha
mashirika yanayotetea haki za binadamu, harakati za rasilimali, utawala bora na
demokrasia, haki za huduma za jamii.
Kutambua nguvu ya kila
taasisi na kutoa sauti na kujenga nguvu za pamoja katika masuala mbalimbali ya
mstakabali wa Taifa, uongozi, ufisadi, harakati za Sheria ya Makosa ya
Kujamiina (SOSPA), iliyoongozwa na TAMWA, na sheria ya Ardhi .
“Mtandao wa Jinsia kutoa
mchango katika mapambano mapana mfano ya ardhi na ya kuhakikisha suala la
jinsia linapewa kipaumbele katika mchakato mzima; ndivyo hivyo hata katika
mchakato wa sasa wa Katiba,” anasema Mallya.
Katika
kipindi hiki TGNP inasema, imeendelea kujitahidi kutoa sauti na msimamo katika kuzungumzia maeneo yenye ukimya
ikiwemo mfumo dume na mwingiliano wake na mfumo wa kiliberali mamboleo; pamoja
na soko huria; suala la UKIMWI na VVU kuwa ni la rasilimali na jinsia.
“Ndio
maana tunatumia fursa mbalimbali kuvunja ukimya kuhusu suala la rushwa ya
ngono, tukihusisha masuala ya mifumo ya kugawa rasilimali inayowapa wachache nafasi zaidi, huku ikipokonya uwezo
wa wengi kujipatia ajira endelevu na zenye hadhi wengi kukosa huduma,” Mallya
anasema.
Anaongeza,
“Hiki ndicho kiini kinachozaa rushwa ya ngono kwa mfano, wanafunzi kutokana na ufinyu
wa mabweni ya kutosha wanafunzi hutozwa hela wakati wa kutaka vyumba kwenye
vyuo na wanafunzi wa kike kudaiwa rushwa ya ngono.”
Mtandao huo kwa mujibu
wa Mallya, unasema lengo hasa ni kudai rushwa ya ngono ili izungumzwe kama
sehemu ya mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini Tanzania, uwajibikaji
kuhusu rushwa ya ngono hususan kupitia kamati za maadili katika taasisi
serikalini, sekta binafsi na nyingine zote ambazo hatuoni zikielekeza nguvu
katika suala hili.
“Lingine ni kuanzishwa
kwa bajeti ya kijinsia kama nyenzo ya kudai na kuelekeza rasilimali fedha
katika kushughulikia haki za wanawake na usawa wa kijinsia. Hii ni nyenzo ya
wanaharakati kudai uwajibikaji, kupata taarifa za mapato na matumizi na
kufuatilia bajeti katika ngazi ya taifa, sekta na serikali za mitaa.”
KURASIMISHA HARAKATI ZA
UKOMBOZI WA WANAWAKE KIMAPINDUZI
Ili kuhakikisha kwa
itikadi na dhamira ya TGNP Mtandao inakuwa endelevu, jitihada kubwa zilifanyika
tangu mwanzo kurasimisha misingi ya harakati hizi katika Sera, mipango,
utaratibu wa utendaji kazi, uwajibikaji wa pamoja na kwa binafsi na zaidi ya
yote katika uongozi wa TGNP Mtandao.
KUNA
CHANGAMOTO GANI?
Changamoto zilizopo ni
pamoja na kuendelea kuzungukwa na muktadha kimfumo, kisera, kisiasa na
kuitamaduni unaoendeleza itikadi ya ubabe, kuendeleza kwa kasi kwa nadharia ya
uzuri wa soko huria wakati upo msimamo wa kuwawezesha wanyonge na hususan
wanawake walioko pembezoni kunufaika zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo
wa TGNP anasema, “Muktadha huu unaongeza nafasi ya kukua kwa mfumo dume katika
ngazi zote na kupunguza fursa za wanaharakati kuleta mabadiliko ya kweli.”
Anasema, “Kwa mfano,
kujengeka kwa tabaka, kuwa wabinafsi zaidi kila mmoja akijaribu kujitafutia
fursa mwenyewe na familia yake, kushusha maonevu kati ya sisi kwa sisi na
kuanza kupigana wenyewe kwa mfano wafugaji na wakulima wadogo wadogo kuchinjana
badala ya kutambua adui mkubwa na kutokutumia fursa za kujenga nguvu za pamoja
kumkabili adui.”
“Kukosekana kwa ajira
endelevu, na kipato cha uhakika na kurudisha majukumu nyumbani kumepelekea
hasira na kuendelea kwa ukatili dhidi ya wanawake hususan kutoka kwa waume au
wapenzi wao.”