Uzinduzi wa kitabu cha Hali Halisi ya Kijinsia Tanzania na Tathimini ya Madai ya Miaka Kumi ya Beijing, huu ni uchambuzi mbadala wa hali ya mahusiano ya Kijinsia Tanzania na mabadaliko muhimu yanayotakiwa katika kufanikisha ukombozi wa wanawake
na usawa wa kijinsia. Kitabu hiki kilizinduliwa rasmi na Mwenyekiti wa FemAct dada Jesca Mkuchu katika viwanja vya TGNP.
Wanaharakati walikuwa na madai matano ambayo yalitokana na utafiti uliozaa kitabu hiki na wanahitaji madai hayo yafanyiwe kazi mapema sambamba na ahadi za serikali.
Madai haya yaliwakilishwa na Mwenyekiti wa Tamwa dada Ananilea Nkya, ambayo ni:
1. Elimu – Wanaharakati wanadai usawa wa 50% kwa 50% kati ya watoto wa kike na kiume katika kupata elimu, Walimu bora, na vitabu kwa wanafunzi wote. Pia wanataka
serikali kukomesha mimba za utotoni ambazo zinakwamisha watoto wa kike kuendele na masomo.
2. Afya – Katika afya wanaharakati wanaitaka serikali itekeleze haraka azimio la Abuja ambalo serikali yetu ililisaini pamoja na nchi zingine za Afrika azimio hilo linazitaka nchi za Afrika kutenga kiasi cha 15% ya bajeti ya nchi zao katika maswala ya afya. Ongezeko hilo litasaidia kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na matatizo ya uzazi.
3. Kazi – Wanaharakati wanadai serikali itekeleze mapendekezo ya mkataba namba 100 wa Shirika la kazi la Mataifa (ILO) linalotaka kuwepo kwa usawa katika ajira kati ya wanaweke na wanaume. Pia wanaharakati wanadai kukomeshwa kwa hali yoyote ya kibaguzi wa kijinsia katika kupandisha vyeo kwa wafanyakazi katika sekta zote binafsi na umma.
4. Kisiasa- Wanaharakati wanadai serikali itekeleze azimio la SADC linalotaka serikali za nchi wanachama kutoa nafasi sawa katika ngazi zote za uongozi kwa wanawake na wanaume kwa asilimia 50% kwa 50%. Pia sambamba na hilo wanataka wanawake watakaopata uongozi waweze kutetea maslahi ya wanawake wenzao.
5. Haki za ujumla kati ya wanawake na wanaume. Katika kipengele hiki wanaharakati wanitaka serikali iondoe sheria ya ndoa ya mwaka 1977 ambayo inanyima mtoto wa kike haki ya kulitumikia taifa hili kwa kuhalalisha ndoa za kuanzia miaka 14.
Dada Mary Rusimbi alifanya hitimisho la nini kifanyike ili kuweza kuleta usawa wa
kijinsia Tanzania, na aligusia swala zima la mgawanyo wa rasilimali Tanzania.
Rasilimali hapa alimaanisha bajeti, Fedha za wafadhili, watu, maliasili n.k. Kwa maoni yake anaona Mgawanyo wa rasilimali haulengi makundi yaliyowekwa pembezoni –vijana, wanawake, na wanaume masikini- badala yake unaendelea kuwanufaisha watu wachache katika jamii kama kipindi cha ukoloni. Pili, Serikali haina mkakati maalumu ?
wa kuwasaidia maskini na wanyonge, na kuwapunguzia kazi wanawake. Tatu, Mikopo midogomidogo-Microfinance- inayotolewa na taasisi za kifedha hazilengi kumkomboa maskini hasa mwanamke bali zinaendeleza unyonyaji kwa jamii. Changamoto ni, tumejizatiti kiasi gani kama taifa katika kuleta mgawanyo unaolingana wa rasilimali za taifa kwa jamii yetu? Uko wapi mkakati wa mgawanyo sawa na wa haki wa rasilimali ya taifa, hasa wenye mrengo wa kuwakomboa wanyonge hasa wanawake?
5 comments:
Binafsi naipongeza sana TGNP kwa jitihada zote inazofanya ili kuleta usawa wa kijinsia katika jamii. Kitabu "Hali Halisi Ya Kijinsia Nchini Tanzania" ni kizuri na kimeweka wazi ukweli ulivyo katika nchi yetu. Na ili kuleta mabadiliko yanayotegemewa ni mpaka pale jamii itakapopata kujuwa Hali Halisi.
Sasa Je Mkakati Gani Umewekwa ili Wananchi wapate kujua yaliyomo ndani ya Kitabu hicho?
Naamini jinsi watu wanavyopata ujumbe ndivyo hisia za ukombozi wa mwanamke kimapinduzi unavyotekelezeka.
Basi kwa namna hiyo, ni vema maudhui hayo yakawekewa mkakati wa kuwafikia wananchi kwa wingi zaidi.
Kwanza napenda kupongeza TNGP kwa hatua iliyofikia na kuweza kuzindua kitabu cha hali halisi ya kijinsia nchini Tanzania. Kwa kweli kitabu hiki kikitumiwa vizuri kitakuwa ni muongozo mzuri wa masuala yote yahusuyo jinsia hapa Tanzania. Hayo madai matano ya wanaharakati kuhusiana na elimu, afya, kazi, siasa na haki za ujumla kati ya wanawake na wanaume ni vyema yakafanyiwa kazi na serikali ili nchi yatu iweze kufikia lengo la usawa wa kijinsia. Naipongeza tena TGNP na mapambano dhidi ya ukombozi wa mwanamke yanaendelea.
Mhhhhhhh!!! Kazi kwelikweli!!!dada Mary Rusimbi mimi naungana na wewe kabisa kwani hakuna mkakati maalum wa kuwakwamua walio wengi. Kama kweli tunataka kuupiga teke umaskini nafikiri kilimo kingepewa umuhimu zaidi kwani asilimia kubwa ya watanzania wako vijijini na ni wakulima hasa wanawake. Waziri mkuu alipotembelea upareni alitoa mfano kuwa kilo moja ya tangawizi ni kama shilingi 250/= lakini tangawizi hiyo hiyo ikisafirishwa kwenda Arusha kilo moja ya tangawizi ya unga ni zaidi ya shilingi 15,000/=Je! huu si unyonyaji wa wazi wa nguvu za maskini hasa wanawake???Upareni kiwanda kinataka kujengwa lakini sehemu nyingine hali ya vijijini ikoje?
Nawapongeza wanaharakati wote kwa jitihada zao za kuleta usawa katika jami hasa wanawake waliowekwa pembezoni. Ni matumaini yangu kwamaba kwa kufanya hivyo itasaidia katika kuleyta maendeleo kwa walengwa husika, nawatakia kila la heri TGNP na wanaharakati wote katika mapambano haya ya yaliyotukuka katika kuleta usawa.
Mwanaharakati.
Ni kitu kizuri na ni ishara ya maendeleo katika harakati za ukombozi. Lakini bado kuna changamoto nyingi mbeleni ambazo wanaharakati wa ukombozi wa wanawake hawana budi kukutana nazo. Kazi njema
Post a Comment