Kipindi cha Longa Mwanaume kinarushwa kila siku ya jumatano na kituo cha ITV, kipindi hiki kinazungumzia mambo mbalimbali ya mahusiano ya wanaume na wanawake -hasa katika ya ndoa. Tangu kiliapoanzishwa -wiki kama tano hivi- kipindi hiki kimekuwa kikijadili mada ambazo zina mlengo wa kuwakandamiza wanawake katika maisha yao ya ndoa, na kujaribu kupaza sauti za wanaume katika jamii au kuonyesha mambo ambayo labda wanaume wanahisi wamepokonywa au wanayoyatakiwa wayashikilie. Hali hii imepelekea wanaharakati kukijadili kipindi hiki katika zama hizi za harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi. Mkanganyiko huo wa maudhui ya kipindi hiki umeibua maswali kadhaa wa kadha ambayo wanaharakati wanaona ni vyema yakajibiwa. Je kipindi hiki ni fursa ama si fursa? Kinaendeshwaje? Au je Kirekebishweje ili kiweze kwenda sawa na harakati hizi za ukombozi wa wanawake kimapinduzi? Maswali hayo na mengine yaliweza kujenga msingi mzima wa mada hii.
Mwezeshaji wa mada hii alikuwa Salma Maulid kutoka Sahiba Sisters Foundation, na alikuwa na maswali makuu manne ya kujadili juu ya kipindi hiki, ambayo ni:
Ni nini madhumuni ya kipindi hiki kulingana na harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi? Wanasemina waliweza kuajdiliana juu ya swali hili na kuafikiana kwamba, kipindi hiki kina lengo la kirudisha nyuma harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika kuleta usawa wa kijinsia katika jamii. Kwa kujadili maswala ya uhusiano wa wanaume na wanawake katika jamii huku wakitoa hoja za kuwakandamiza wanawake na kuacha maswala ya msingi yanayoikabili jamii yetu hasa katika kuleta usawa wa kijinsia ni wazi waongozaji wa kipindi hiki wana lengo la kurudisha nyuma harakati zinazoendelea za ukombozi wa wanawake.
Kwa nini kipindi hiki kimekuja sasa wakati vuguvugu la harakati za wanawake kimpinduzi limepamba moto? Hapa majibu mawili yalipatikana, la kwanza; labda meseji ya harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi zimewafikia wale wasiopenda mabadiliko hivyo wakatafuta mbinu ya kujihami mapema kabla mabadiliko kamili hayajatokea. La pili; labda kipindi hiki ni mojawapo ya njia za wasiopenda mabadiliko kukwepa hoja pana ya upiganaji dhidi ya mfumo dume kwa kuibua matatizo madogo-madogo yanayowahusu wanawake hasa katika mahusiano ya kindoa, ili kupotosha dhana nzima ya mapamabano dhidi ya mfumo dume.
Je ipo mijadala mengine inayoendelea huku pembeni inayofanana na hii? Mijadala mingine inayofanana na hii bado ipo katika jamii yetu, washiriki wa semina walitoa mfano wa kipindi kimoja cha redio ambacho kilikuwa kinajadili juu ya watoto wanaopata mimba wakati wakiwa shuleni na hitimisho la kipindi hiko lilikuwa wanafunzi hao wafukuzwe shule moja kwa moja. Pia matangazo ya biashara ya shirika moja la Simu za mkononi na Benki fulani hapa nchini ambayo yote yalihusisha utoaji wa mahali kubwa kwa wasichana waliotaka kuolewa, hii inaendelea kuonyesha wasichana bado wanaonekana kuwa ni vitu ambavyo vinaweza kununuliwa kwa kiasi fulani cha fedha. Matangazo na mijadala kama hii inachangia kurudisha nyuma harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi zinazoendeshwa na wanaharakati wapenda mabadiliko kote duniani.
Je Longa mwanaume Kinazungumzia Maswala ya wanaume? Kipindi hiki cha longa mwanaume hakizungumzii maswala ya msingi yanayowakabili wanaume na wanawake wa Wakitanzania wa leo, badala yake kimekuwa kikijadili vitu ambavyo si muhimu na kuacha maswala muhimu yanayohusu jamii yetu. Kwa mfano, kinashindwa kujadili maswala ya ajira, makazi bora, huduma za afya, kuondoa tofauti za kijinsia na kuleta usawa katika jamii, na vita dhidi ya rushwa. Hivyo kipindi hiki kimekazania kujadili mambo ya mzaha na yasiyokuwa na faida katika jamii yetu hasa kwa mustakabali wa kizazi kijacho.
Kwa kuhitimisha, Wanasemina walipendekza kipindi hiki cha Longa Mwanamume kifanyiwe marekebisho ili kiweze kutoa fursa kwa jamii inayolenga kuleta mabadiliko ya usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake kimapinduzi. Mada na uongozaji wa kipindi hiki urekebishwe ili uweze kutoa fursa kwa ujenzi wa jamii mpya yenye usawa wa kijinsia na yenye kumthamini mwanamke.
2 comments:
ahsante kwa mada hii.nachopenda kuchangia ni vizuri kumuita huyu mratibu wa kipind hicho aeleze kwa malengo yake na dira ya kipind hicho ili tupate mwanga na kufanyia marekebish.
ni vizuri kama tungempata anayeendesha kipindi hiki ili aje kutoa maelezo zaidi ni kwa nini anaendesha kipindi kama hiki labda anaweza akawa na maana yake.
asante.
Post a Comment