Mada hii iliwakilishwa na Kamishina wa Polisi, Bi. E.A Mapunda Mkuu wa chuo cha polisi Kurasini tarehe 30/06/2008 na kuibua hoja motomoto kutoka kwa washiriki wa semina. Jeshi la polisi lipo katika mabadiliko makubwa ya kuboreshwa huduma zake kwa jamii kwa lengo la kupambana na uhalifu pamoja na ukatili wa kijinsia. Mabadiliko hayo yalianza mwaka julai 2006, na yana mihimili mikuu mitatu ambayo ni Polisi jamii, weledi (Professionalism-kuzingatia maadili, taaluma na viwango vilivyowekwa), na usasa (modenization-kuboresha rasilimali watu, vitendea kazi, ofisi, makazi, na maslahi ya askari). Misingi mengine ni pamoja na maboresho ya sekta ya sheria, sekta ya fedha, na maboresho yanayoendana na serikali ya mtaa.
Polisi jamii inalenga kujenga mazingira endelevu ya kuliwezesha jeshi la polisi kufanya kazi pamoja na jamii hasa kudumisha amani. Falsafa hii imejijenga katika nguzo kuu nne ambazo ni; kuwepo kwa mashaurino kati ya polisi na jamii, kutatua matatizo au kero, kuwepo marekebisho au mabadiliko, na kuwepo na uhamisishaji.
Katika kuenenda na mabadiliko haya, tarehe 25/10/2007 jeshi la polisi liliunda Mtandao Wa Polisi Wanawake (Tanzania Police Female Network) kwa lengo la kupamna na uhalifu wa makosa yanayohusiana na ukatili wa kijinsia. Uongozi wa Mtandao huu upo katika ngazi zote kuanzia taifa hadi wilayani katika mikoa yote bara na visiwani.
Dira, Dhima na Madhumuni ya Mtandao wa Polisi.
Dira: kuwa chombo cha utendaji cha kitaalam katika kutoa huduma bora na kuongeza ufanisi katika kazi za polisi.
Dhima: kujenga na kudumisha mshikamano miongoni mwa polisi wanawake, askari wengine na jamii ili kudumisha mahusiano na kuwa karibu na wananchi na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma.
Madhumuni: Kuondoa hofu ndani ya jamii dhidi ya jeshi la polisi, kuliweka jeshi la polisi karibu na jamii hasa wanawake ili kuweza kupata taarifa zaidi za uhalifu na wahalifu, kushirikiana na wananchi kwa karibu katika kuyatambua na kuyatatua matishio ya uhalifu yanayowakabili katika maeneo wanayoishi, kubadilishana mawazo na wananchi ni jinsi gani wanaweza kulisaidia jeshi la polisi katika kuwatambua na kudhibiti uhalifu, kusimamia na kukemea suala zima la unyanyasaji wa wanafunzi katika daladala, na kuelimisha jamii juu ya baadhi ya vitendo vinavyoashiria makosa ya jinai ikiwemo ukatili wa kijinsia.
Mtandao umefanikiwa kutoa mafunzo ya ukatili wa kijinsia kwa maofisa, wakaguzi na askari 180 kutoka vituo 18 vya kanda ya Dar es salaam na katika vyuo vyote vya polisi na mafunzo haya yatakuwa ni endelevu. Kuendelea kutoa mafunzo katika shule za msingi mkoa wa Dar es salaam kata ya Kurasini katika somo linaloitwa Usalama Wetu, na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kazi za mtandao.
Mtandao unakabiliwa na Changamato/Matatizo zifuatazo; raia wengi wanashindwa kugundua ukatili wanaofanyiwa kama una asili ya kijinsia, mila na desturi za badhi ya makabila zinachangia ukatili wa kijinsia, na mtazamo wa jamii kwa polisi bado hauridhishi.
Matarajio ya mtandao huu ni pamoja na; kuwa na dawati katika vituo vya polisi la kusikiliza matatizo ya ukatili wa kijinsia katika mikoa yote ya Tanzania, kuendelea kupata mafunzo zaidi ili kuboresha azima ya jeshi la polisi, na kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa dawati hili na kuwa tayari kutoa ushirkiano pale wanapopata matatizo.
Wana-GDSS walipendekeza Dawati hili lipelekwe katika vyombo vya habari ili wananchi wengi zaidi waweze kufahamu, zifanyike juhudi ya kuongeza idadi ya askari wanawake, urasimu katika vituo vya polisi ukomeshwe, wananchi wafikishe taarifa za ukatili wa kijinsia na uhalifu mwingine katika vituo vya polisi na vyombo husika, na jeshi la polisi liwe na mkakati maalumu wa kutetea rasilimali za wananchi wa Tanzania dhidi ya mabepari/wawekezaji.
Kwa kuhitimisha, jeshi la polisi lina safari ndefu ya kuelimisha jamii ili liweze kupata ushirikiano zaidi kutokana na dhana zilizojikita miongoni mwa raia wengi kwa sababu ya manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa askri wa jeshi hilo. Uboreshwaji huu unaweza ukafungua ukurasa mpya katika kuelekea jamii bora ya Kitanzania bila uhalifu. Tanzania bila uhalifu inawezekana!
2 comments:
Ninashukuru mbinu hii inaweza kuleta mabadiliko katika kupambana na uhalifu lakini kuna haja sana ya kuongeza mapambano dhidi ya uhalifu. Kwa hali jinsi ilivyo jeshi letu la polisi limeshapoteza zamani mahusiano mema na wananchi hivyo kazi ya kurudisha imani ni kubwa sana.
jeshi letu la polisi limepoteza uaminifu kwa raia kwa sababu mara nyingi wamekuwa wakipendelea sana rushwa na kipindi kingine wamekuwa wakiwatetea wahalifu ili mradi wamepatiwa kitu kidogo hata kama sio wote wenyewe tabia mbaya lakini mara nyingi watu hupenda kujumuisha wote kama ni wabaya....
bado wanayo kazi kubwa sana
Post a Comment