MUUNGANO wa Wanahabari Tanzania (Tajoa), umeanza kutekeleza programu yake ya kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya Watanzania wanapata habari hasa zinazoandikwa magazetini.
Katika programu yake hiyo yenye jina la HakiHabari, Tajoa imetoa magazeti 100 kwa wafungwa wa Gereza la Wilaya ya Njombe jana na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Gereza hilo kwa niaba ya wafungwa wanaotumikia vifungo vya muda tofauti katika gereza hilo.
Akizungumza jana wakati wa kukabidhi magazeti hayo, Mwenyekiti wa Tajoa, Simon Mkina, alisema muungano huo wa waandishi wa habari na marafiki, wametoa magazeti hayo bure ikiwa ni mwanzo wa mkakati wake wa kutoa magazeti na habari kwa wafungwa hao kila wiki.
Mkina alisema Tajoa imeamua kuwahabarisha wafungwa kwa kuwapa magazeti 100 kila wiki, huku muungano ukiwa na utaratibu wa kuandika habari zote muhimu duniani na kuwasambazia wafungwa.
"Tumeanza na Gereza la Njombe, na tunasonga kwenye magereza mengine, ambapo tutakuwa tukigawa magazeti na kijarida cha jumuiko kinachoitwa HakiHabari kila wiki kwa wafungwa, kwa kuanzia wale wa Njombe na baadaye mikoa ya jirani , ikiwa nafasi ya rasilimali itaruhusu," aliongeza Mkina.
Mkuu wa Gereza hilo, Fortunatus Ntani aliishukuru Tajoa kwa kuamua kuanzisha utaratibu huo ambao aliuita ni chachu ya maendeleo ya elimu na ufahamu kwa wafungwa, kwani nao wana haki ya kuhabarishwa hata kama wako magerezani.
Akieleza sababu za kuanzishwa kwa Tajoa, Mkina aliliambia gazeti hili kwamba yeye na waandishi wengine zaidi ya 10 waliamua kuanzisha jumuiko hilo kwa lengo la kutoa msaada kwa waandishi wenyewe na Watanzania, walioko pembezoni au wale wasiofikiwa na habari kirahisi.
Mkina alisema waandishi, pamoja na kufanya kazi nzuri ya kupigania neema kwa Watanzania, wao wamekuwa ni kundi linalojisahau kudai haki zao, ikiwa ni pamoja mazingira bora ya kazi, ujira na vitendea kazi.
"Sisi waandishi tumekuwa tukijisahau sana, tunazungumzia sana shida na matatizo ya wengine, wakati nasi tumo katika mazingira hayo hayo ya wale tunaowapigania, na sasa tunaona wakati umefika kupigania haki zetu, na Tajoa ni daraja la kufanya kazi hiyo," alisema Mkina.
Naye Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Tajoa, Fredy Kihwele alisema mbali na programu ya HakiHabari, Tajoa pia inatekeleza majukumu yake kupitia programu zingine tatu; Sema, Mwalimu na Saidia.
Akifafanua programu hizo, Kihwele alisema Sema inahusika na kuibua mijadala ili wananchi waizungumzie na kutoa mawazo yao, Mwalimu inahusika na kuwajengea uwezo waandishi kwa njia za mafunzo mbalimbali na Saidia ni programu ya kusaidia waandishi kiuchumi na hali wanapopata matatizo wakiwa kazini au vinginevyo.