Monday, March 26, 2012

Kampeni za lala salama Arumeru

WIKI ya kampeni za lala salama inaanza leo katika Uchaguzi Mdogo wa Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, huku ushindani mkubwa ukionekana zaidi kwa mgombea wa CCM, Sioi Sumari na wa Chadema, Joshua Nasari.

Tayari vyama vimeanza kujipanga kwa kampeni hizo kwa kupeleka viongozi wake na kufanya mikutano mingi ya wazi na ya ndani kushawishi wananchi kuchagua wagombea wao katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo, Aprili mosi mwaka huu.

Wakati kila chama kikijipanga, CCM ambacho kimethibitisha kuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ndiye atakayefunga kampeni zao, kimedai kunasa barua ya siri ya Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, akieleza wasiwasi wa chama hicho kushindwa katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa madai ya CCM, Dk. Slaa katika barua hiyo anawashutumu viongozi wa kampeni za Chadema kwamba wamekuwa wakitumia lugha chafu za matusi, kumkashifu Mkapa na kuendesha kampeni zisizo za kistaarabu hatua ambayo inakiweka chama hicho katika mazingira ya kushindwa kwenye uchaguzi huo.

Meneja Kampeni wa CCM katika uchaguzi huo, Mwigulu Nchemba alionesha barua hiyo mbele ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha King’ori jimboni Arumeru Mashariki.

“Ndugu wananchi hata kabla ya uchaguzi kufika tayari Chadema wameanza kukiri kushindwa katika uchaguzi. Ushahidi wa hili ni hii barua iliyoandikwa na Dk. Slaa akilaumu uendeshaji wa kampeni zisizo za kistaarabu hatua anayosema itakifanya chama hicho kushindwa.

“Anawaambia; ‘kwa vile tulikubaliana kufanya kampeni za kistaarabu nyie mmekiuka makubaliano hayo na kuendesha kampeni chafu za kuwatukana wananchi, kuwakashifu viongozi wakiwemo Rais Mkapa, Stephen Wasira (Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM), na viongozi wengine.

“Mbali ya kashfa hizo pia mmekuwa mkitoa lugha za matusi zinazowaudhi wananchi wa Arumeru. Suala hili limewafanya wazee kuchukizwa na mikutano ya kampeni ya Chadema na ni dhahiri kwamba kwa mwenendo huu kuna uwezekano mkubwa kwa mgombea wetu kushindwa,” alidai Nchemba akinukuu barua hiyo anayodai kuwa ya Dk. Slaa.

Alidai pamoja na hayo, barua hiyo inawaagiza Mameneja Kampeni wa Chadema (Vincent Nyerere- Mbunge wa Musoma Mjini na Mchungaji Izraeli Natse – Mbunge wa Karatu) kuwaandaa vijana ili kufanya fujo kupinga matokeo endapo mgombea wa CCM, Sioi atatangazwa mshindi.

Nchemba alidai kutokana na maagizo hayo tayari Chadema wamewaingiza jimboni hapa, vijana wanaounda kundi linalojulikana kama Mungiki ili kufanya fujo siku ya kutangaza matokeo. Alidai kundi hilo liliendesha vurugu ikiwa ni pamoja na kummwagia mwanaCCM mmoja tindikali katika Uchaguzi Mdogo wa Igunga.

“Ndugu wananchi nawaambieni wazi Chadema si chama cha siasa hiki ni chama cha watu wanaopenda fujo na vurugu. Endapo siku moja Chadema itakuja kushika madaraka ya kuongoza, nchi hii haitatawalika itakuwa vitani wakati wote,” alidai Nchemba.

CCM pia imeongeza idadi ya mikutano ya ndani na nje inayofanywa na jumuiya zote za chama hicho, Jumuiya ya Wazazi, Umoja wa Vijana (UVCCM) na Jumuiya ya Wanawake (UWT) katika kumnadi Sioi.

No comments: