Tuesday, March 13, 2012

JK: Madaktari Niaminini

RAIS Jakaya Kikwete amewashukuru madaktari kwa kumwamini na kurejea kazini na kuwaahidi kushughulikia madai yao na kuyapatia ufumbuzi yote ambayo Serikali itakuwa na uwezo nayo.

Pia kuhusu kuondolewa kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu
wake, Dk Lucy Nkya, amesema viongozi hao hawakuchukuliwa hatua kwa kuwa hakupewa tuhuma zozote zinazowakabili.

Pamoja na hayo, Rais Kikwete amewashangaa wanaharakati waliojitokeza katika kipindi chote
cha mgomo wa madaktari na kuilaumu Serikali, badala ya kutumia nafasi zao kutetea maisha
ya Watanzania ambayo yalikuwa hatarini kutokana na mgomo huo.

Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam jana, aliwataka madaktari hao kumwamini na
kumwachia kazi ya kushughulikia madai yao na kusisitiza kuwa mgomo huo usijirudie na badala yake taaluma na Sheria za nchi vizingatiwe.

“Nawashukuru madaktari kwa kuniamini na kurejea kazini, lakini pia nawaomba waniamini, ninawahakikishia kuwa tunawathamini na kuwajali na tutafanya yale yote yaliyo chini ya
uwezo wetu, yatakayotushinda hatuwezi kuwaahidi ila tutajitahidi,”alisema Rais Kikwete.

Alisema tangu mgomo huo uanze Desemba mwaka jana, kwa madaktari walio mafunzoni kugoma wakidai posho zilizocheleweshwa na baadaye Chama cha Madaktari Tanzania
(MAT) kuingilia na kuja na madai mapya likiwamo la nyongeza ya mishahara, Serikali haikubweteka na imekuwa ikijitahidi kwa hali na mali kuzuia mgomo huo.

Alisema mara kadhaa vimefanyika vikao vya madaktari na upande wa Serikali na madaktari
kuja na madai ya nyongeza ya mishahara, posho ya mwezi, posho ya mazingira magumu,
posho ya mazingira hatarishi, posho ya usafiri na bima ya afya, ambapo madai mengine kupitia Tume iliyoundwa na Serikali yalianza kushughulikiwa.

Alisema pamoja na hayo hali iligeuka ambapo katika vikao vya mwisho baina ya madaktari hao na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hawakujitokeza na katika kikao cha mwisho na maofisa wa Wizara ya Afya, walitoa masharti ya saa 72 kwa Rais ya kutaka Dk Mponda na Dk Nkya waondolewe ndipo waendelee na mazungumzo.

Alifafanua kuwa baada ya Serikali kuona hali ni mbaya kwa upande wa wananchi, iliamua kupeleka suala hilo katika Tume ya Usuluhishi na baadaye Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi lakini upande wa madaktari haukuhudhuria sehemu zote mbili.

“Ndipo Mahakama ilipotoa amri kwamba mgomo uliokuwa unaendelea ni batili na kuwataka warejee kazini, ukweli ni kwamba hapa nchini sheria ipo inayozuia sekta muhimu ikiwamo ya afya, idara ya maji na umeme kugoma na si hapa nchini tu hata nchi nyingine duniani,” alisema.

Alisema katika nchi nyingine sheria zao ni kali zaidi kwani iwapo daktari atasababisha kifo
cha mgonjwa kwa kugoma, hushitakiwa kwa tuhuma za kuua bila kukusudia.

“Sheria hii kwetu ipo lakini haina masharti haya wala hatutarajii kuyaweka.” Aliwataka madaktari kutambua kuwa kazi yao haifanani na kazi nyingine, kwani wanapogoma waathirika wakubwa huwa ni wananchi ambao hupoteza maisha.

“Dereva wa daladala akigoma athari ni watu kutembea kwa miguu lakini si kupoteza maisha, nawaomba huu uwe mgomo wa mwisho zingatieni taaluma yenu na sheria za nchi.”

Hata hivyo, alisema pamoja na juhudi zote hizo madaktari hao walikutanishwa na maaskofu wa
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na ndipo walipokutana na Rais Kikwete na kufikia
makubaliano ya kuendelea na mazungumzo huku wakiwa wamerejea kazini.

Rais Kikwete aliahidi kutowaangusha madaktari hao kwani tayari suala lao la nyongeza ya posho limepitishwa na kinachosubiriwa ni majibu kutoka Hazina, lakini pia aliwasisitiza
wakati mazungumzo yakiendelea waepuke kuipa Serikali masharti kwa kuwa siku zote
wanaozungumza hawagombani.

Kuhusu mawaziri alisema jambo la msingi si kuwasimamisha viongozi hao ila ni kuhakikisha
mambo ya msingi yanafanyiwa kazi, kwani kiuhalisia mawaziri ni viongozi wa kisiasa, ambao hupita tu katika wizara.

Alisema pamoja na kwamba mgomo huo umekwisha na suala hilo kuendelea kushughulikiwa,
amejifunza kuwa kuna tatizo kubwa la pande mbili kutoamiana, hali iliyosababisha kutokea kwa mgomo huo ulioleta maafa kwa watu wasio na hatia.

“Jambo la kusikitisha katika mgomo huu wapo wengine walioingilia, si mnajua adui yako
mwombee njaa, wanaharakati walisimama na kuzungumza mengi, sawa tunayapokea, lakini
kama wao ni watetea haki za binadamu hivi jamani kuna haki kubwa zaidi ya maisha ya watu?”
Alihoji.

Alisema wanaharakati hao walikuwa na wajibu wa kujitokeza na kukemea mgomo huo kwa
manufaa ya maisha ya Watanzania, matokeo yake walitumia fursa hiyo ya matatizo ya Watanzania kujitafutia umaarufu.

Kuhusu sekta ya afya alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuiboresha ambapo imeongeza bajeti
mara sita tangu Uhuru kutoka Sh bilioni mbili hadi Sh trilioni 1.2, imejenga zahanati kila kata na vituo vya afya, imeboresha vyuo ili kuongeza udahili na kupandisha mishahara ya madaktari na wauguzi.

No comments: