Wednesday, February 17, 2010

Kambi za Lowassa, Sitta zadaiwa kuipasua CCM

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Pius Msekwa amesema, semi zenye maudhui ya upatanishi zilitumiwa na Kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuzipatanisha kambi mbili za wabunge wa CCM zilizosigana ndani ya Bunge kwa muda mrefu.

Amezitaja kambi hizo kuwa ni ile iliyokuwa ikiongozwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta na ya Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.

Msekwa amewaeleza waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa,Kamati ya Mwinyi imefanya kazi nzuri ya kutafuta kiini cha mpasuko miongoni mwa wabunge wa CCM ndani ya Bunge kama ilivyotumwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho.

Amesema,Kamati ya Mwinyi ilikutana na wabunge wa CCM kwa siku nne mfululizo kuanzia Novemba mosi hadi Novemba nne, mwaka jana mjini Dodoma na kuzungumza nao ili kudadisi kiini cha mpasuko baina yao bungeni.

Kutokana na maelezo ya wabunge hao wa CCM, Kamati ya Mwinyi ilibaini kuwa kulikuwa na makundi, la Lowassa na la Sitta, chanzo kikiwa ni hofu kutoka kila upande kuwa mwenzake ana mpango wa kumng’oa.

“Kutokana na maelezo yao, ilionekana kuwa uhasama hasa ulianza baada ya ripoti ya Richmond kuwasilishwa bungeni ambapo yaliibuka makundi hayo mawili yaliyoanza kushambuliana, kundi moja likiitwa la mafisadi na lingine likijiita la upambanaji dhidi ya ufisadi,” amesema Msekwa.

Msekwa amesema,kutokana na malumbano hayo, kila kundi liliingiwa na hofu kuhusu kundi lingine kuendesha mikakati ya chini chini ya kuwaondoa wenzao madarakani.

“Hawa wanaodai kupambana na ufisadi walianza kulalamika kuwa kundi la mafisadi lilikuwa linawatumia watu ili kuwang’oa katika ubunge kwa kumwaga mabilioni ya fedha kwa watu hao na kundi la pili lilikuwa likilalamika kwa kubatizwa jina la mafisadi, jina ambalo kimsingi linamaanisha rushwa, jambo ambalo ni kosa kisheria,” alisema.

Msekwa amesema,baada ya kubaini hilo, Kamati ilizungumza na kila kundi kwa nyakati tofauti kujadili namna nzuri ya kuondoa tofauti baina yao.

“Kimsingi hali sasa ni shwari, lakini bado ipo kazi ambayo imebakia na tumeiomba NEC ituongeze muda ili tuifanye, nayo ni ya kukutanisha makundi hayo na vinara wao (Sitta na Lowassa) ili wote watoe madukuduku yao mbele ya wenzao na kuhitimisha uhasama. Kazi hii tutaifanya karibuni na tutaleta taarifa katika kikao cha NEC mwezi ujao,” alisema Msekwa.

Amesema,Kamati ilibaini kuwa malumbano hayo yalipamba moto zaidi kutokana na Kamati ya Wabunge wa CCM kutofanya vikao kama kanuni zinavyoelekeza na hivyo wabunge kuligeuza Bunge kuwa sehemu ya kushambuliana badala ya kutumia vikao vya Kamati ya Wabunge wa CCM.

Alisema Kamati ilipochunguza kama kulikuwa na uendeshaji mbovu wa shughuli za Bunge chini ya Spika Sitta na kuwa chanzo cha malumbano hayo, Kamati hiyo ikiwajumuisha watalaamu wa zamani wa uspika (Msekwa-Spika Bunge la Tanzania na Abdulrahman Kinana – Spika Bunge la Afrika Mashariki), ilibaini kuwa Sitta alikuwa akiendesha Bunge kwa kuzingatia kanuni na sheria za Bunge bila kupotosha hata kidogo.

“Hata hivyo wao wenyewe (Wabunge wa CCM) walionesha wasiwasi kuhusu baadhi ya kanuni za Bunge kuwa inawezekana zikachangia malumbano hayo, lakini tuliwaambia kwa kutumia vikao vyao vya Bunge, wanaweza kuziangalia kanuni hizo kuona kama wanaweza kuzirekebisha kwa namna watakavyo bila kuingiliwa,” amesema.

Hata hivyo, alisema ishara iliyoonekana katika kikao cha Bunge kilichopita ambapo wabunge na Sitta walifunga rasmi mjadala wa Richmond ndani ya Bunge bila kushinikizwa, inaonesha kuwa Kamati hiyo imeanza kupata mafanikio makubwa ya kujenga umoja na mshikamano baina ya wanaCCM hao.

Alisema Kamati hiyo pia iliridhishwa na namna wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walivyokuwa wakijadili masuala yanayowasilishwa katika Baraza hilo ili kujadiliwa.

No comments: