Tuesday, August 16, 2011

Wabunge walia na Katibu Mkuu Ardhi

WABUNGE wamemtaja Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, kuwa kikwazo cha utatuzi wa masuala ya ardhi hasa migogoro kuhusu uwekezaji na kutaka aondolewe, la sivyo hakuna kitakachofanikiwa.

Wabunge wamesema hayo wakati wa mjadala wa Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2011/12 yaliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Aliyeanza kuchangia hoja alikuwa Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu (CCM) ambaye kabla ya kutoa hoja, alijisafisha kuhusu tuhuma za Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC) akisema hahusiki kwa namna yoyote na sakata hilo, hivyo wapiga kura wake wasihofu.

“Kabla ya kuchangia naomba kusema jambo, kutokana na maneno yaliyozagaa, mimi huko kwenye DDC sipo kabisa, kwani mwaka 2009 aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani, aliunda Tume inayofanya shughuli zote za DDC, mimi sipo, hizo ni kelele za mpangaji hazimyimi usingizi mwenye nyumba,” alisema Mtemvu.

Alipomaliza kujisafisha kuhusu DDC, Mtemvu alichangia kuhusu hotuba kwa kubainisha wazi kuwa haungi mkono hoja kwa kuwa hana majibu kuhusu mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, eneo la Kurasini licha ya maagizo kutolewa na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, watu walipwe stahili zao lakini bila mafanikio.

Mtemvu alisema hata Waziri Tibaijuka alitembelea eneo hilo na kuahidi kuwa wanaopisha mradi tangu mwaka 2006 watalipwa, lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea na kwa wachache waliolipwa, walilipwa fidia ya Sh 300,000 kwa msingi na kati ya Sh milioni moja hadi 4.5 kwa ardhi na nyumba.

“Waziri wala Naibu Waziri hawana shida, tatizo lipo kwa Katibu Mkuu wa hii wizara na kama ataendelea kukaa katika nafasi hiyo, kazi yote nzuri ya Waziri itakuwa ni bure, kwa kuwa hakuna kitakachofanyika, “Napata hofu kubwa na mradi wa Kigamboni, kama serikali itaweza kwa hali hii, kama hakuna fedha, watu waelezwe ili waendelee kujenga,” alisema Mtemvu huku akishangiliwa hasa na wabunge wa upinzani.

Mbunge wa Mkinga, Dastan Kitandula (CCM), akichangia hoja, alisema suala la uwekezaji limekuwa sumu kwa wazawa, kwa kuwa limewathamini zaidi wageni na inatishia amani kwa kuwa baadhi yao wamepewa maeneo ya mipakani suala ambalo ni la hatari.

Kitandula alitolea mfano jimboni kwake, akisema kuna hekta 25,833 walizopewa wawekezaji mchanganyiko (wazawa na wageni likiwamo Jeshi la Kujenga taifa (JKT), lakini katika kile alichokiita kichekesho na jambo la kusikitisha, hekta nyingine 25,000 zimetolewa kwa mwekezaji mmoja, aliyemtaja kuwa ni Mwitaliano mwenye kampuni ya Arkadia Limited ili alime mibono.

Kitandula alisema wananchi wa wilaya hiyo hawana tatizo na wawekezaji kwa kuwa hao 11 hawajapata tatizo lolote, lakini wamemtaka kutounga mkono hoja hasa kutokana na ukweli kuwa, katika eneo la Mkinga lenye hekta 250,000 mwekezaji mmoja ana hekta 25,000.

Alisema anashangazwa na utendaji kazi wa wizara zinazohusika na ardhi ikiwemo TAMISEMI, lakini hasa Katibu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambaye katika barua yake (tunayo) aliyoiandika Julai 2 na kupokewa Mkinga Julai 4, aliridhia kwamba mwekezaji huyo apewe ardhi hiyo huku Katibu wa TAMISEMI akiandika naye barua ya kuzuia.

“Huu ni mkanganyiko, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi anaidhinisha mwekezaji huyu apewe eneo hilo la hekta 25,000 na barua nyingine kutoka Katibu Mkuu TAMISEMI inazuia uuzwaji huo, hiki ni nini?

Inasikitisha zaidi kwa kuwa wawekezaji wazawa wananyimwa nafasi na kupewa Wazungu,” alisema Kitandula.

Alisema ana wasiwasi kuwa baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wanampotosha Rais Jakaya Kikwete na kumsababisha aonekane mbaya kwa wananchi wa Mkinga kutokana na uzembe wa wachache na kumtaka Waziri Tibaijuka alishughulikie hilo.

Wabunge wengine waliochangia mjadala huo katika kipindi cha asubuhi ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) ambaye alitaka suala la ardhi liwe haki kwa kila Mtanzania hasa wakulima wa pamba wa Shinyanga.

Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Chatanda (CCM) alitaka maofisa ardhi wawajibishwe kwa kuwa wamekuwa chanzo cha kugawa ardhi na kutaka maeneo yote ya wazi yarejeshwe serikalini.

Katika hatua nyingine, Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee (Chadema), ametaja baadhi ya vigogo nchini kuwa wanamiliki ardhi kinyume cha utaratibu na kuwa kikwazo kwa maendeleo ya wananchi.

Waliotajwa na Msemaji huyo jana bungeni ni Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM, John Malecela.

Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula na Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika Awamu ya Tatu.

Akitoa hotuba ya kambi hiyo ya bajeti ya mwaka 2010/11 ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mdee alisema migogoro mingi ya ardhi imeshindwa kutatuliwa kutokana na nguvu ya wakubwa kama hao.

Alidai vigogo hao wanamiliki mamia kwa maelfu ya hekta katika maeneo yanayotakiwa kupewa wanakijiji wa Wami katika shamba la lililokuwa Shirika la Usimamizi wa Ranchi za Taifa (NARCO) wilayani Mvomero, Morogoro.

“Shamba hili (la NARCO) lina ukubwa wa hekta 49,981 na taarifa zinaonesha hekta 30,007 ilipewa kampuni ya Sukari ya Mtibwa licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa eneo ni kubwa.

“Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa maeneo yaliyokuwa yagawiwe kwa wanakijiji, wamepewa wananchi wafuatao:“Mangula ana hekta 2,000, Malecela hekta 100, Ngwilizi hekta 5,000 zilizosemwa wamepewa wakulima wadogowadogo wa kijiji.

“Mwinyi hekta 2,000, Sumaye hekta 500 na Mkapa hekta 1,000,” alisema Mdee.

Hata hivyo, alimwondoa Mkapa katika tuhuma hizo za shamba namba 299 kwa kuwa ameliendeleza tofauti na viongozi hao wengine aliowataja katika hotuba yake.

Kambi hiyo ya upinzani ilihoji kama vigogo hao ni wanakijiji wa Wami-Dakawa na ni vigezo gani katika utaratibu uliowahusu wanakijiji, vilitumika kuwapa mashamba na kuwanyima wanakijiji wengine.

Pia alihoji kama Serikali haioni mgao huo umejaa dhuluma na upendeleo unaohatarisha maisha ya Watanzania na usalama wa nchi kwa jumla.

Alidai wananchi wana hasira, kwa kuwa walishaelezwa kuwa watapata hekta tano kila mmoja baada ya kutozwa Sh. 20,000 kila mmoja na hivi sasa kwa mujibu wa Mdee, wanaelezwa kuwa maeneo hayo yamekwisha.

No comments: