Friday, November 27, 2009

Uzinduzi wa Siku 16 Za Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake Duniani tarehe 25 na 26 Novemba 2009 - Viwanja vya Mnazi Mmoja na Karimjee.

Wasemavyo Waliohudhuria Katika Uzinduzi wa Siku 16 Za Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake Duniani - Viwanja vya Mnazi Mmoja na Karimjee.


Said Nyanja – GDSS Mabibo.
Mambo yanayozungumziwa katika makongamano kama haya ni yale ni yale, inabidi wanaharakati kuweka mikakati zaidi ya kuweza kuboresha matukio kama haya. Watu waliohudhuria ni wachache na wahusika wakuu -wanawake wanaonyanyaswa- hawapo katika kongamano hili. Hivyo kupelekea ujumbe kuwafikia watu wachache, ambao pia sio wahusika wakuu wa manyanyaso hayo tunayoyapinga! Wanaharakati wanatakiwa wajipange zaidi ili waweze kuwafikia na kuzishirikisha taasisi za mikoani hasa zinazotetea haki za akina mama, pia ni vyema tukafikilia kuwashirikisha wanafunzi na camp -vikundi vya vijana vya mitaani- ili kuweza kufikisha taarifa na ujumbe huu majumbani na mitaani kwa watu wengi zaidi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Prudenciana Otaro – House of Peace.

Jamii haijafahamu umuhimu wa kushiriki katika matukio kama haya, ipo haja ya kuzishirikisha zaidi jamii na familia. Wanaharakati tuna kazi ya kutoa elimu zaidi, badala ya kuendelea kugawa vipeperushi ambavyo pia ni nadra kwa wanajamii kuvisoma. Ni vyema kama wanajamii wanao hudhuria katika maonyesho kama haya wangepata bahati ya kueleweshwa juu ya kazi za mashirika mbalimbali kabla ya kugawiwa vipeperuhi, ambavyo vingi vimekuwa vimeandikwa katika lugha ya kigeni. Ipo haja ya kuongeza elimu zaidi kwa jamii juu ya siku hizi 16, matangazo mitaani na mashuleni ili wananchi wengi waelewe zaidi juu ya harakati hizi zinazoendelea. Pia ni muhimu sana kwa wanaharakati kuanza kubadilisha mtazimo wao na kuangalia jinsi ya kufanya harakati kama hizi katika mikoa mingine tofauti na sasa ambapo harakati hizi zinafanyika Dar es salaam peke yake na huku watu wenye shida hizi za manyanyaso wapo mikoani zaidi ya hapa mjini. Huku mijini mahudhurio sio mazuri ukilinganisha na shughuli kama hizi zikifanyika mikoani.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Mama Nuru Mtewele na Mama Jona Jonas - WOFATA

Watu wengi hawana taarifa za kitu kama hiki, hata wanaokuja hapa katika mazimisho haya hawajui kwa nini wanakuja katika kitu kama hiki. Pia kwa sisi, wajasiriamali ni kazi ngumu kufika katika maeneo kama haya. Ni vizuri waandaji wakafanya utaratibu kuandaa matukio kama haya maeneo ambayo ni karibu na wananchi ili iwe rahisi kwa wajasiriamali kuwakilisha bidhaa zao. Pia ni vyema siku hii ijulikane kitaifa kama zilivyo siku ya UKIMWI au siku ya akina mama duniani ili iweze kuwa na heshima tofauti na sasa ambapo bado haijapewa hadhi wakati ni siku muhimu sana katika harakati za kuwakomboa akina mama na wajasiriamali kama sisi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Dickens Mwakibolwa na Isabela Nchimbi – NOLA

Uzinduzi umefanikiwa kwa maana ya kuweza kukusanya watu wengi katika viwanja vya mnazi mmoja, lakini inaonekana watu wengi waliohudhuria walishindwa kutumia fursa zilizopo katika uzinduzi huo. Kwa mfano kwa sisi tunaotoa huduma za kisheria tulitegemea kupata watu wengi wa kuwasaidia katika uzinduzi huu, lakini badala yake tumepata watu watatu tu kwa kutwa nzima na tunaamini wapo watu wengi sana wenye shida ya huduma ya kisheria. Wananchi wengi hawana uelewa juu ya kitu kama hiki. Wanafunzi waliletwa katika maandamano bila kuelimishwa wanakuja kufanya nini, ni vyema wakaelimishwa kabisa mashuleni kabla ya kuja katika shughuli kama hizi ili waweze kutumia fursa watakazokutanazo huku. Pia jana katika uzinduzi makada wa chama cha mapinduzi(CCM) walikuja kwa wingi ambao kwa kweli hawakufahamu umuhimu wa siku hii. Ni vyema kwa wakati ujao wanaharakati wakaangalia aina ya wageni rasmi wa shughuli kama hizi, na kuepukan na wageni wa kisiasa ambao wanakuwa na itifaki nyingi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Pia Chinyele na Edna Lushaka -LHRC
Uzinduzi umefanikiwa kwa kiasi chake, siku ya kwanza kulikuwa na watu wengi zaidi, hivyo wengi tunatarajia meseji iliweza kuwafikia watu wengi zaidi. Mapungufu yalikuwepo hasa baada ya mgeni rasmi Mh. M Pinda kuchelewa kufika uwanjani na kusababisha wanafunzi na wanaharakati kukaa juani kwa muda mrefu sana jambo ambalo ni hatari hasa kwa wototo wa shule. Pia watu wengi hawafahamu juu ya siku hizi 16 za ukatili dhidi ya wanawake, ama ukatili dhidi ya wanawake una maana gani na ni nini umuhimu wa kutomeza ukatili huu. Upo umuhimu wa kuwafundisha zaidi watoto na wanafunzi kuliko kuwavalisha ma-tshirt. Pia watu walishindwa kutumia fursa za misaada ya kisheria zilizokuwepo katika viwanja vya uzinduzi kwa sababu walishindwa kufahamu kwamba kuna huduma kama hizo katika viwanja hivyo. Wanaharakati tunahitaji kutumia mbinu mbadala kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii juu ya siku kama hizi, badala ya kutumia luninga, redio na magazeti peke yake, ni vyema kama tukitumia vitu kama matarumbeta na midundiko ambavyo vinaweza kuwavuta wananchi wengi zaidi na kufikisha ujumbe kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Immaculata Moria na Joel Swebe -Tawla

Mwamko wa jamii bado ni mdogo sana na bado shughuli kama hizi zinafanyika Dare s salaam pekee wakati watu wengi wenye shida za ukandamizaji wapo mikoani na vijijini, ipo haja kwa wanaharakati kuangalia zaidi maeneo hayo ya vijijini. Ipo haja ya kubadilisha mfumo wa kutangaza shughuli kama hizi, badala ya kutumia vyomba vya habari kam magazeti, redio au luninga ni vyema tukatumia mbinu za maigizo na ngoma za asili kama midundiko na mdumange. Pia ni bora shughuli kama hizi tukazizindulia maeneo ya watu wa chini badala ya viwanja kama hivi vya mnazi mmoja na karimjee ambapo wananchi wa hali ya chini hawawezi kuhudhuria kwa urahisi.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Hadija Zuberi, Kuruthum Rashid, na Fatuma Kandambovu - SIYODE Manzese, Sisi kwa Sisi.

Kwetu sisi, siku hii ni muhimu sana kwa ajili ya kujifunza zaidi juu ya harakati hizi za ukombozi wa wanawake Tanzania, kwani sisi ni wanaharakati wageni na tumeunda kikundi chetu baada ya kuja mara kwa mara pale katika semina za GDSS Mabibo. Tunatarajia tutakachokipata hapa tutakipeleka kwa wenzetu ambao hawajapata bahati ya kuja katika viwanja hivi. Ila wenzetu wengi hawana habari juu ya semina hizi ni vyema waandaaji wakatoa matangazo zaidi hasa maeneo ya kwetu ambapo watu wengi hawasomi magazeti wala kuangalia taarifa za habari mara kwa mara. Sisi wenyewe hatuna uelewa wa kutosha juu ya siku hii, kitu ambacho kinafanya tushindwe kushiriki kikamilifu zadi. Lakini tunashukuru kama tutahudhuria vitu hivi mara kwa mara vinaweza kutufungua akili zetu zaidi na zaidi na kuweza kuwakomboa pia na wenzetu, kwani kwa kweli bado wanawake tunanyanyaswa bila kujua!

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Nuru Lukusasi – Mwanachama wa GDSS

Muda wa siku mbili kwa ajili ya uzinduzi ni mdogo ukilinganisha na matatizo wanayokutana nayo wanawake katika jamii hii. Ni vyema waandaaji wakaangalia jinsi ya kutafuta rasilimali ya kutosha ili waweze kufanya kongamano la muda mrefu zadi, hata wiki moja na wanawake wengi waweze kutoa visa mkasa vyao na kuchangia hoja mbalimbanli na machungu wanayokutana nayo katika jamii kuliko ilivyo sasa, ambapo katika muda wa siku mbili tu uzinduzi unafanyika. Wanawake hawafahamu juu ya taarifa hizi za Karimjee na faida ya kuhudhuria sehemu kama hizi, kwa mfano, mimi mwenyewe nimeambiwa leo kuhusu kufanyika kwa kitu kama hiki. Kama ningefahamu mapema ningeweza kuwachukua na wanawake wenzangu na kuja nao hapa kwa sababu wao ndio wanaofahamu hasa manyanyaso wanayoyapata! Maeneo na shughuli kama hizi ni muhimu kwa wanawake kuhudhuria kwani pamoja na kujifunza mambo mengi pia yanapunguza uoga na kuongeza ujasiri hasa kwa sie wanawake tuliosoma zamani!

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dai, Chukua Hatua, Pinga Ukatili wa Kijinsia.

2 comments:

Anonymous said...

poleni wanaharakati, tunahitaji nguvu ya pamoja kusukuma jahazi hili, tutafika tukishirikiana zaidi ya hivi tunavyofanya sasa. Changamoto zilizpo zitutie moyo zaidi. kila la kheri.

Anonymous said...

poleni wanaharakati, tunahitaji nguvu ya pamoja kusukuma jahazi hili, tutafika tukishirikiana zaidi ya hivi tunavyofanya sasa. Changamoto zilizpo zitutie moyo zaidi. kila la kheri.