Friday, March 13, 2009

Mrejesho wa Kamati ya GDSS Iliyoundwa kufuatilia Mkutano wa IMF na Afrika

Mrejesho na kamati iliyoundwa tarehe 18/2/2009 ili kufikisha mawazo mbadala kwa Serikali, Shirika la Fedha Duniani(IMF) na washirika wao kutoka kwa Wanaharakati wa Maendeleo na Jinsia na wananchi kwa ujumla kuhusu zahama/mgogoro wa uchumi duniani na kufanyika kwa mkutano wa IMF nchini tarehe 10–11/3/2009. Katibu wa kamati hiyo Hashim Luanda alisema, kimsingi kamati hiyo kwa kushirikiana na asasi nyingine za kiraia (AZAKI) walipanga kufanya maandamano pamoja na kuandaa tamko maalumu na kulifikisha kwa walengwa.

MATOKEO YA KAMATI
Kupitia mwamvuli wa Policy Forum, Human Development Trust (HDT) na Tanzania AIDs Forum, kamati ya GDSS kwa pamoja na asasi nyingine za kiraia za ki-Tanzania walikutana katika ukumbi wa Dar es salaam International Conference Center (DICC) na kutoa tamko lenye madai yafuatayo:-
• Kuitaka IMF kushirikisha wadau katika utungaji sera za uchumi kwa nchi husika na kupinga sera za jumla kwa makundi mbalimbali ya nchi kwa sababu ya utofauti wa mazingira.
• IMF ipunguze/kulegeza masharti yake kwa kuzingatia maoni ya wadau kwa kuzishauri nchi kuunda sera ambazo mahitaji ya watu wake. Mfano: Iruhusu serikali iweze kutumia fedha ipatazo kutoka kwa wafadhili kwa kuwekeza katika miradi ya maendeleo nchini badala ya kuzitumia katika kuongeza akiba ya fedha za nje.
• Kuitaka serikali ya Tanzania ibadili mtazamo wake kwa wadau wa maendeleo nchini kwa kutoa kipaumbele kwa AZAKI katika kutunga, kuridhia, kusimamia na kutathmini sera za uchumi wa nchi na hatimaye kuzifanya sera za uchumi kuwa mali ya wananchi.
• Kuitaka serikali kutoa fursa ya ushirikishwaji katika ngazi mbalimbali za mipango na utekelezaji wake ili kukidhi mahitaji ya wananchi. Mfano: Katika Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) ambao unaangalia na kusimamia mapambano dhidi ya umasikini.
• Kuitaka serikali kupunguza pengo kubwa lililopo kati ya “Walionacho” na “Wasionacho” ili kupunguza uwezekano wa nchi kuingia katika machafuko yatakayosababishwa na kukata tamaa kwa wananchi walio na kipato cha chini.

Katibu wa kamati alisema, hawakufanikiwa kuandaa maandamano kutoka na ufinyu wa muda na badala yake kamati ya GDSS ilishiriki katika mkutano mbadala kuhusu zahama / mgogoro wa uchumi duniani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa British Council ambao pia uliratibiwa na asasi zilizotajwa hapo awali.
Mkutano huo ambao ulishirikisha wanaharakati, wataalam wa uchumi na wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salam (UDSM) na Mzumbe, ulijadili kwa kina ili kupata takwimu sahihi katika ukuaji/kuanguka kwa uchumi nchini.

Mwisho alisema, katika mambo yote waliyoshiriki walipata mapokeo mazuri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini na kuelezea matumaini ya kamati yake kuwa ujumbe utawafikia walengwa. Hivyo aliwataka wananchi kwa ujumla wao kutumia fursa ya msukumo ambao uliooneshwa na wanaharakati ili kuongeza nguvu katika kuihoji serikali katika ngazi mbalimbali za uongozi.

Ripoti imetayarishwa na Ally Nindi.

2 comments:

Anonymous said...

wanaharakati maazimio haya tunayoyafikia mara kwa mara ni vizuri kama tungeletewa na mrejesho wake ili tujue tumepiga hatua kiasi gani? ni vizuri kuwa na mfumo wa kujipima ni kiasi gani malengo yetu yamefikiwa.
Mdau

Anonymous said...

ni kweli kamati bila mrejesho ama maazimio bila mirejesho ya kueleweka, haviwezi kutusaidia kitu tunahitaji mirejesho hai kwa kila kamati ama maazimio tunayofikia.

kila la kheri.